Dhaira |
Na Mahmoud Zubeiry
HALI ya kipa wa Simba SC, Abbel Dhaira inaendelea vizuri na
leo jioni anaweza kuanza mazoezi kwenye Uwanja wa Sigara, Chang’ombe, Dar es
Salaam.
Msemaji wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wataangalia
leo jioni kama Dhaira ataweza kufanya mazoezi baada ya kupewa mapumziko ya siku
tatu.
“Baada ya mapumziko ya jana, timu leo inaanza mazoezi, kwa
hivyo tutaangalia Dhaira kama atakuwa katika nafasi ya kufanya mazoezi, baada
ya kupumzika kwa siku tatu,”alisema Kamwaga.
Kipa huyo namba moja wa Uganda, hakuingizwa kwenye programu ya
mechi ya kwanza ya timu yake ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara juzi dhidi ya African Lyon kutokana na maumivu ya nyonga.
Katika mchezo huo, ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao
3-1, ‘Tanzania One’ Juma Kaseja alianza langoni na kufanya kazi nzuri, ikiwemo
kuokoa mkwaju wa penalti ya Shamte Ally.
Hata hivyo, refa Israel Mujuni aliyetoa penalti hiyo
baada ya beki Paul Ngalema kumkwatua Fred Lewis, aliamuru irudiwe kwa madai Kaseja
alitokea kabla ya mpira kupigwa na safari hiyo mpigaji akapiga nje kabisa.
Kamwaga alisema hata kiungo Mganda ambaye sasa anarudishwa
kucheza nafasi ya ulinzi, Mussa Mudde alitolewa kipindi cha pili kwenye mechi
dhidi ya Lyon, kutokana na kuumia misuli, hivyo naye ataangaliwa pia jioni ya
leo kama atakuwa kwenye nafasi ya kufanya mazoezi.
Aidha, Kamgwa alisema kikosi cha Simba SC kinarudi kambini
leo, katika hoteli maridadi na adilifu ya Sapphire, iliyopo Kariakoo, Dar es
Salaam, kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu, dhidi ya JKT Ruvu, Februari 3,
mwaka huu.