Abbel Dhaira |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA namba
moja wa Uganda, Abbel Dhaira anatarajiwa kuwasili leo saa 8:00 mchana kujiunga
na klabu yake mpya, Simba SC ya Dar es Salaam, akitokea kwao Uganda.
Dhaira aliyesaini
mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya dola za Kimarekani 40,000, na mshahara
wa Sh. Mlioni 2 kwa mwezi, baada ya kutua Dar es Salaam atakwenda moja kwa moja
Zanzibar, ambako Simba itashiriki Kombe la Mapinduzi.
Kikosi kizima
cha Simba, kasoro Nahodha Juma Kaseja, Emmanuel Okwi, Amir Maftah na Amri
Kiemba kitaondoka leo mchana kwenda Zanzibar, tayari kwa michuano ya Mapinduzi.
Dhaira aliyeibukia
Express ya Uganda mwaka 2006, mwaka 2008 alihamia U.R.A. pia ya Uganda, ambayo
aliichezea hadi mwaka 2010 alipohamia Ulaya.
Kwa kumpata
Dhaira, Simba SC imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza,
Juma Kaseja ambaye amekuwa akisoteshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo
inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha
uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi
za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja
alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha
mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili
katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu
hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema
hataki tena kuchezea Simba.
Lakini
pamoja na matatizo hayo, Kaseja ameendelea kuitwa kwenye kikosi cha timu ya
taifa ambako ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa
ukweli.