Bin Kleb |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI
wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kwamba
tuzo aliyopewa kwenye Mkutano wa Jumapili ni kwa ajili ya watu wote ambao
amekuwa akifanya nao kazi bega kwa bega katika kuijenga klabu hiyo.
Bin Kleb
alipewa tuzo ya kiongozi mwenye mchango mkubwa ndani ya Yanga katika mkutano wa
Jumapili, Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam kutokana na
mchango wake wenye kuonekana katika klabu hiyo.
Hata hivyo, Mtanzania
huyo mwenye asili ya Kiarabu alisema kwamba ingawa yeye anaonekana anafanya
kazi kubwa Yanga, lakini wapo watu ambao amekuwa akishirikiana nao na pengine
wakifanya makubwa zaidi kuliko yeye, lakini ama hawaonekani au hawapendi
kuonekana.
Bin Kleb alisema
kwamba hadi kufikia hapa Yanga imerejesha heshma yake kuna watu ambao wamefanya
kazi kubwa pamoja na Kamati ya Utendaji kwa ujumla, Baraza la Wadhamini na Kamati
zote zilizoundwa.
“Kwenye
Kamati yangu pekee kuna watu kama Beda Tindwa, Isaac Chanji, Mussa Katabaro na
wengineo, lakini kuna watu ambao pia wamefanya kazi kubwa sana, tena sana
pengine kuliko hata mimi, watu kama Seif Ahmad, Davis Mosha,Majjid Suleiman,Hussein Nyika na wengineo ambao
hawapendi kutajwa, hakika wana mchango mkubwa sana Yanga,”alisema Bin Kleb.
Aidha, Bin Kleb
ameomba ushirikiano kwa wana Yanga ili kuhakikisha timu inaendelea kufanya
vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unaoanza
Jumamosi.
“Kuongoza
Ligi si maana yake tumechukua ubingwa, tunatakiwa kuendeleza mshikamano ambao ulileta
mafanikiko haya, ili tufanikishe azma ya kutwaa ubingwa na pia kulipa kisasi
cha 6-0 kwa watani wetu, Simba SC,”alisema Kleb.
Yanga
ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa pointi
zake 29, baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na Azam iliyomaliza na pointi
zake 24 na mabingwa watetezi, Simba SC waliomaliza na pointi 23.