Abdi Kassim |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
ABDI Kassim
Sadallah ‘Babbi’ au Ballack wa Unguja yuko mbioni kuihama klabu ya Azam FC na
kurejea na Mtibwa Sugar ya Morogoro, kutokana na kushindwa kuvumilia kuwekwa
benchi chini ya kocha Muingereza, Stewart Hall.
BIN ZUBEIRY inafahamu Babbi tayari yupo kwenye
mazungumzo na Mtibwa Sugar, klabu yake ya kwanza kuchezea Tanzania Bara, ambayo
imeonyesha nia ya kumpokea tena.
Babbi
amekuwa akilalamika kwa watu wake wa karibu kwamba, wakati wa kocha Mserbia
Boris Bunjak alikuwa anapangwa Azam na kufanya vizuri kiasi cha kuisaidia sana
timu, lakini baada ya kurejea Stewart amekuwa mtu wa benchi.
Babbi
amekuwa akisema Azam ilipokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwezi
uliopita kwenye Kombe la Hisani, alipangwa katika mechi mbili za mwanzo ambazo
Stewart alibaki Kenya kwa kukosa viza ya kuingia Kinshasa.
Amekuwa
akilalamika kwamba pamoja na kucheza vizuri katika mechi hizo, maisha
yalibadilika ghafla baada ya Stewart kutua Kinshasa, kwani kuanzia hapo
hakumbuki kama alivaa tena hata jezi ya Azam hadi mashindano yanaisha.
Habari zaidi
zinasema, tayari Babbi amekwishawaeleza nia yake ya kuondoka baadhi ya viongozi
wa Azam, ambao wameonekana kukosa namna ya kumzuia, kwa sababu nao wanaona ana
sababu ya kufikia uamuzi huo, kunusuru kiwango chake.
Azam ipo
visiwani hapa kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi, lakini katika mchezo wa jana
dhidi ya Coastal Union alikuwa sehemu ya watazamaji jukwaani.