Na Bin Zubeiry |
WAKATI tunaelekea ukingoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara, wachezaji wanne wa klabu ya Azam FC walisimamishwa na
klabu yao kwa muda usiojulikana kwa tuhuma zilizowekwa wazi, za kuihujumu timu
hiyo katika mechi dhidi ya Simba SC.
Azam walisema hivyo, ingawa hadi leo wameshindwa kuthibitisha
madai yao na wachezaji hao tangu wakati huo hawajahusishwa katika programu
yoyote ya timu hiyo.
Hao ni kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Aggrey Morris
aliyekuwa Nahodha, Erasto Nyoni na Said Mourad.
Hizi ni habari za kawaida sana kusikia katika soka ya
Tanzania, mchezaji kahujumu mechi imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku katika
mpira wetu.
Ukitazama kwa undani sana, utagundua haya mambo hayazungumzwi
hivi hivi tu, ni kweli yapo katika soka yetu na msimu uliopita yalitawala sana.
Mbaya zaidi, kuna wakati hata watu wa klabu moja wanaweza
kuhujumiana wao wenyewe, kwa kuwahonga fedha wachezaji wao wacheze chini ya
kiwango ili watimize malengo, kama kuung’oa uongozi uliopo madarakani na
kadhalika.
Wakati haya yanaendelea, tunashuhudia soka yetu ikizidi
kudidimia kila siku na mifano iko wazi, kwamba sasa shabiki wa soka wa Tanzania
hana ndoto ya kushuhudia mafanikio ambayo klabu zefu zilipata miaka ya nyuma.
Mara ya mwisho Simba SC kufanya vizuri katika michuano ya
Afrika ilikuwa mwaka 2003 walipofuzu kucheza hatua ya makundi, wakati kwa
wapinzani wao, Yanga ilikuwa mwaka 1998.
Azam ni timu ngeni na ingawa imo kwenye mbio za ubingwa kwa
misimu mitatu sasa, lakini bado inapewa muda kulingana na uchanga wake.
Timu zote tatu zilizo katika mbio za ubingwa, zimekuwa
zikihusishwa katika mchezo mchafu. Simba wananawashika uchawi Azam na Yanga,
Azam wanawashika uchawi Simba na Yanga, Yanga wanawashika uchawi Azam na Simba.
Huo ndio umekuwa mwenendo wa soka yetu katika miaka ya
karibuni, ingawa mizizi ya haya mambo ilianzia wakati ule mwanzoni mwa miaka ya
1990, wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia walipovamia kwa kasi katika klabu
hizi.
Mwishoni mwa miaka ya 1990 walitoweka na kidogo soka yetu
ikaanza kujiumba upya, lakini ghafla yamerudi tena, tena kwa kasi na mafundi ni
sisi wenyewe tunaojiita wazalendo.
Ukweli ni kwamba, kama kweli tunaipenda soka yetu lazima
tupambane na rushwa ili kumlinda mchezaji na soka yetu kwa ujumla. Tukatazane
kushawishi wachezaji kwa hongo na tuhimizane kucheza soka kwa matokeo halisi ya
uwanjani.
Wakati hatua ya lala salama ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
inaanza mwishoni mwa wiki, timu zote tatu zilizo katika mbio za ubingwa
zinaonekana kuwa na maandalizi mazuri.
Yanga walikwenda kambini Uturuki kwa wiki mbili, ambako
pamoja na kujifua ufukweni, gym na uwanjani, walipata mechi tatu za kujipima
nguvu.
Katika mechi hizo tatu, dhidi ya Ariminia Bielefed ya Daraja la Nne Ujerumani
waliyotoka nayo sare ya 1-1, kabla ya kufungwa 2-1 na Denizlispor FC ya Daraja la Kwanza Uturuki
na 2-0 na Emmen FC ya
Daraja la Kwanza Uholanzi.
Na
waliporejea, walipata mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Black Leopard ya Afrika
Kusini na kushinda mabao 3-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Leo tena
wanarudiana na Leopard Uwanja wa Kirumba, Mwanza.
Ikumbukwe
Yanga ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa
pointi zake 29, baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na Azam iliyomaliza na
pointi zake 24 na mabingwa watetezi, Simba SC waliomaliza na pointi 23.
Azam
wanarejea leo kutoka Kenya, ambako walicheza mechi tatu za kujipima nguvu,
dhidi ya timu ya Benki ya Biashara Kenya, KCB waliyoifunga bao 1-0 sawa na
Sofapaka wakati mchezo wake wa kwanza, mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi
walifungwa mabao 2-1 na AFC Leopard.
Awali ya
hapo, Azam walikwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako walicheza
Kombe la Hisani na kufanikiwa kulitwaa. Waliporudi, wakaenda Zanzibar kwenye
Kombe la Mapinduzi, ambako walicheza na kushinda taji hilo.
Simba SC
inarejea leo kutoka Oman ilipoweka kambi ya wiki mbili na kupata mechi tatu za
kujipima nguvu, wakishinda moja dhidi ya Ahly Sidab mabao 2-1 na kufungwa
mbili, 2-1 dhidi ya U23 ya Oman na 3-1 dhidi ya timu ya Jeshi la nchi hiyo,
Qaboos.
Kesho watacheza
na Black Leopard Taifa. Awali ya hapo, Simba SC ilikwenda Zanzibar kwenye Kombe
la Mapinduzi, ambako walitolewa katika Nusu Fainali na Azam kwa mikwaju ya
penalti, baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 120.
Ukizungumzia
maandalizi, hakika timu zote tatu zilizo katika mbio za ubingwa zimejiandaa
vema na zimeonyesha dhamira ya kushindania ubingwa. Timu zote zina makocha wa
kigeni, tena Wazungu ambao tunaamini ndio bora.
Makocha hawa
wanalipwa fedha nyingi. Timu zote zimesajili wachezaji bora hadi wa kigeni,
tena ambao wana namba kwenye vikosi vya timu zao za taifa. Wachezaji wote wana
mikataba ya malipo mazuri. Wanalipwa vizuri.
Baada ya
haya yote haya, dhahiri mashabiki wa soka nchini na wadau kwa ujumla wanasubiri
kushuhudia ushindani halisi, utakaotokana na namna ambavyo timu ziliwekeza
katika maandalizi.
Tunataka
kuona wachezaji na makocha wanaitumikia mishahara na marupurupu yao uwanjani na
si kusikia eti, mchezaji fulani alihongwa akafungisha. Hapana. Wakati umefika
sasa, tuachane na haya mambo na tucheze soka.
Kuna faida
gani kuwa na kocha wa kigeni, wachezaji watano wa kigeni, na hata wa hapa hapa,
kuchagua wale walio bora na kuwalipa vizuri, halafu unakwenda kuhonga mchezaji
wa timu pinzani ili ushinde?
Nafurahia
sana ujio wa Bodi ya Ligi Kuu yenye sura na dira mpya, nitasema nao
wakikamilisha mambo yao, ila kwa sasa naomba niwasihi hawa farasi watatu
wanaofukuzana kwenye mbio za ubingwa, Azam, Simba na Yanga, tunataka kushuhudia
walichovuna katika maandalizi yao, na si ufundi wa kununua mechi. Alamsiki.