Mwaikimba akipongezwa na Himid Mao baada ya kufunga |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
AZAM FC
imefufua matumaini ya kutetea Kombe la Mapinduzi, baada ya usiku huu kuilaza
Miembeni ya hapa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa.
Kwa matokeo
hayo, Azam imefikisha pointi nne na kupanda kileleni mwa Kundi B, ikifuatiwa na
Miembeni yenye pointi tatu, Coastal Union ya Tanga pointi mbili na Mtibwa Sugar
yenye pointi moja inashika mkia.
Hadi
mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa mabao 2-1. Azam walikuwa wa kwanza kupata
bao dakika ya pili lililofungwa na beki Mkenya, Joackins Atudo akiunganisha kwa
kichwa kona ya kiungo Mkenya, Humphrey Mieno.
Miembeni
walisawazisha bao hilo dakika mbili tu baadaye, baada ya kona iliyochongwa na
Adeyoum Saleh kuingia moja kwa moja nyavuni, kutokana na jitihada za
mshambuliaji mkongwe, Monja Liseki kumbana kipa Mwadini Ally asiufikie mpira.
Baada ya bao
hilo, Azam walicharuka na kuzidisha kasi ya mashambulizi langoni mwa Miembeni,
jambo ambalo liliwasaidia kupata bao la pili dakika ya 34 baada ya mshambuliaji
Gaudence Mwaikimba kuinasa pasi maridadi ya Mieno na kusogea nayo mbele kidogo
kabla ya kumchambua kipa Suleiman Hamad.
Baada ya
refa Ally Omar Kisaka kupuliza kipyenga cha kuashiria kutimu kwa dakika 45 za
kipindi cha kwanza, makocha wa timu zote, Muingereza Stewaert Hall wa Azam na
Salum Bausi walimfuata mwamuzi huyo kumzonga kwa madai ya kuchezeha ovyo.
Kipindi cha
pili, refa huyo aliporejea kabla ya kuanzisha mchezo, aliwapa kadi nyekundu
makocha wote.
Ikiongozwa na
Kocha Msaidizi, Muingereza Kali Ongala, Azam ilipata bao lake la tatu dakika ya
87, mfungaji Uhuru Suleiman aliyeuwahi mpira uliorudishwa na beki kufuatia
Gaudence Mwaikimba kutaka kufunga kwa kichwa.
Katika
mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samir Hajji
Nuhu, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Salum Abubakar/Jabir Aziz dk
82, Humphrey Mieno/Ibrahim Mwaipopo dk 83, Gaudence Mwaikimba, Brian Umony/Abdallah
Seif dk60 na Hamisi Mcha ‘Vialli’/Uhuru Seleman dk 65.
Miembeni FC;
Suleiman Hamad, Mfaume Odello, Adeyoum Saleh, Salum Hajji, Salum Juma, Sabri
Ally/Adam Hamisi dk 70, Laurent Mugiya, Suleiman Hajji, Monja Liseki/Mohamed
Hamdan dk45, Rashid Roshwa/Peter Ilunda dk62 na Issa Othman.
Katika
mchezo wa kwanza, Coastal Union ya Tanga ililazimishwa sare ya kufungana bao
1-1 na Mtibwa Sugar ya Morogoro, katika mchezo wa Kundi B Kombe la Mapinduzi,
jioni hii kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa.
Hadi
mapumziko, hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Coastal Union
ndio walitakiwa kujilaumu kwa kushindwa kutumia mwanya wa Mtibwa Sugar kucheza
pungufu kutokana na beki wake, Salum Swedi kutolewa nje kwa kadi nyekundu
dakika ya 43.
Timu zilishambuliana
kwa zamu katika kipindi hicho, upande wa Coastal ukiongozwa na Danny Lyanga na
Mtibwa Hussein Javu.
Baada ya
Swedi kutolewa nje kwa kadi nyekundu, kocha Mecky Mexime alimuinua beki Rajab
Mohamed kwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji, Hassan Seif.
Kipindi cha
pili, Mtibwa walirudi kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya
58, mfungaji Ally Mohamed ‘Gaucho’ aliyepiga shuti la umbali wa mita 19 na
kumtungua Juma Mpongo.
Coastal
Union ilisawazisha bao hilo dakika ya 81, mfungaji Jerry Santo aliyefumua shuti
la chini la umbali wa mita 24 na kumtungua kipa Hussein Sharrif.
Katika
mchezo huo, kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Hussein Sharrif, Hamisi Issa,
Yussuf Nguya, Salvatory Ntebe, Salum Swedi, Babu Ally Seif, Ally Mohamed
‘Gaucho’, Rashid Gumbo, Hussein Javu, Hassan Seif/Rajab Mohamed dk43 na Vincent
Barnabas.
Coastal
Union; Juma Mpongo, Ismail Khamis, Othman Tamim, Philip Metusela, Mbwana Khamis
‘Kibacha’, Hamisi Shengo, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Jerry Santo, Mohamed
Miraj, Mohamed Soud Othman na Danny Lyanga.