Shujaa wa Azam leo, Mwaipopo |
Na Prince Akbar
AZAM FC ya
Dar es Salaam imemaliza vema ziara yake ya wiki moja nchini Kenya, baada ya
kuifunga timu ya Benki ya Biashara Kenya, KCB bao 1-0 kwenye Uwanja wa City, Nairobi
jioni hii.
Bao pekee la
ushindi la Azam jioni hii limefungwa na kiungo Ibrahim Mwaipopo kwa shuti la
mpira wa adhabu katika dakika ya pili ya muda wa nyongeza, baada ya kutimu kwa
dakika 45 za kawaida za kipindi cha kwanza.
Hata hivyo,
Azam ingeweza kuondoka na ushindi mnene zaidi leo, kama si kiungo wake mwingine
Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ kukosa penalti dakika ya 83 baada ya shuti lake la
kudakwa na kipa wa KCB.
Huo unakuwa
ushindi wa pili katika mechi zake tatu za kujipima nguvu nchini humo, kwani
awali bao pekee la Gaudence Exavery Mwaikimba kwa penalti dakika ya 58 juzi liliipa
Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Sofapaka ya Kenya kwenye Uwanja wa Nyayo,
Nairobi, Kenya.
Katika mchezo
wake wa kwanza, mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi walifungwa mabao 2-1 na AFC
Leopard kwenye Uwanja huo huo wa Nyayo.
Pamoja na
kufungwa na Leopard, Azam watajilaumu wenyewe, kwani walipoteza penalti mbili
kupitia kwa Joackins Atudo na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Mabao ya Leopard
katika mchezo huo, yalifungwa na Paul Were na Mike Barasa, wakati la Azam
lilifungwa na Sammih Hajji Nuhu kwa penalti.
Katika
mchezo wa leo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Malika Ndeule, Samir
Hajji Nuhu, David Mwantika/Omar Mtaki, Joackins Atudo, Kipre Balou/Abdulhalim Humud,
Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo/Humphrey Mieno, Abdi Kassim, Brian Umony/Uhuru Suleiman
na Khamis Mcha/Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Azam kesho
watapanda basi lao kuvuka boda la Namanga kurejea nyumbani Dar es Salaam,
tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.