Kikosi cha Azam |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
MICHUANO ya
Kombe la Mapinduzi inatarajiwa kuendelea leo visiwani hapa kwa mechi mbili za
Kundi B kupigwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Mtibwa Sugar
kutoka Morogoro wataanza kushuka dimbani kumenyana na Coastal Union ya Tanga
saa 10:30 jioni kwenye Uwanja huo, kabla ya mabingwa watetezi, Azam kumenyana
na Miembeni SC saa 2:30 usiku.
Mechi zote
zinatarajiwa kuwa kali na za kusisimua, kutokana na matokeo ya awali ya timu
zote.
Mtibwa walifungwa
4-1 na Miembeni katika mchezo wa kwanza na ili kufufua matumaini ya kubaki katika
michuano hii watatakiwa kushinda leo. Coastal walilazimishwa sare ya bila
kufungana na Azam FC katika mchezo wa kwanza, hivyo nao watahitaji ushindi
kuweka hai matumaini ya kuendelea na Kombe la Mapinduzi.
Azam na
Miembeni, hiyo ni mechi inayotarajiwa kuteka hisia za wengi zaidi leo visiwani
hapa, kwani timu zote ziko madhubuti.
Miembeni imeimarishwa
upya kwa usajili kamambe chini ya kocha Salim Bausi, aliyeiwezesha Zanzibar
kushika nafasi ya tatu kwenye Kombe la Challenge mjini Kampala, Uganda mwezi
uliopita wakati Azam pamoja na kuwa mabingwa watetezi wa Kombe hilo, ndiyo
yenye kuvutia hisia za wengi Bara baada ya Simba na Yanga.
Kikosi cha Coastal |