Abdallah Juma akishangilia kwa kuonyesha maandishi kwenye fulana yake baada ya kufunga penalti ya mwisho usiku huu |
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
ZANZIBAR
imekufa kiume, baada ya kutolewa kwa penalti 4-2 na Kenya katika Robo Fainali
ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kwenye
Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika ya
120.
Hadi
mapumziko, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, Zanzibar wakitangulia kupata
bao dakika ya 20, mfungaji Khamis Mcha ‘Vialli’, aliyeunganisha pasi ya Jaku
Juma, baada ya kazi nzuri ya Suleiman Kassim ‘Selembe’.
Kenya
ilisawazisha dakika ya 29, mfungaji Mike Barasa ambaye alifumua shuti
lililowachanganya Nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kipa wake, Mwadini Ally
na kutinga nyavuni.
Zanzibar
waliuanza vizuri mchezo huo na kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa
Kenya kutokea pembeni, ambao walionekana kabisa kuzidiwa na kutumia muda mwingi
kucheza kwa kujihami.
Hata hivyo,
baada ya kupata bao la kusawazisha, kibao kiliwageukia Wazanzibar na kuanzia
hapo Kenya ndio waliokuwa wakisukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa
wapinzani wao.
Kipindi cha
pili, mchezo ulianza kwa kasi na Zanzibar walionekana kucheza kwa tahadhari
wakiwadhibiti Wakenya, huku wakiendelea kumiliki zaidi mpira.
Hali hiyo
ilizaa matunda ya Heroes kupata penalti dakika ya 75 baada ya mshambuliaji Juma
Jaku kuangushwa kwenye eneo la hatari, Joackins Atudo, wakati anakwenda kumuona
kipa Duncan Ochieng na refa Thierry Nkurunzinza wa Burundi akaamuru pigo hilo.
Nahodha
Aggrey Morris alikwenda kupiga penalti hiyo na kuikwamihsa kimiani kuipatia bao
la pili Zanzibar.
Hata hivyo,
bao hilo halikudumu sana, kwani dakika ya 80 Kenya walisawazisha kupitia kwa
Mike Barasa tena, akiunganisha krosi ya Paul Were aliyeingia kuchukua nafasi ya
Ramadhan Mohamed dakika ya 46.
Hadi dakika
90, timu hizo zilikuwa zimefungana 2-2 na mchezo ukahamia kwenye dakika 30 za
nyongeza, ambako Kenya walishinda.
Khamis Mcha
‘Vialli’ alikosa penalti ya kwanza kabisa na Issa Othamn Ally akakosa ya pili,
wakati Aggrey Morris na Samir Hajji Nuhu walifunga. Kwa upande wa Kenya,
waliofunga ni Mike Barasa, Joackins Atudo, Edwin Lavatsa na Abdallah Juma
aliyepiga ya mwisho.
Kwa ushindi
huo, Kenya itacheza Fainali na mshindi wa mechi ya pili kati ya Uganda na
Tanzania, wakati Zanzibar itawania nafasi ya tatu dhidi ya timu itakayofungwa
usiku huu.
Kenya; Duncan
Ochieng, Anthony ‘Modo’ Kimani, Joackins Otieno Atudo, David Owino Odhiambo,
Abdallah Juma Baya, David Ochieng, Kevin Omondi Obwaka, Humphrey Ochieng Mieno,
Clifton Miheso Ayisi/Paul Were Ooko, Ramadhan Mohamed Salim/Edwin Lavatsa Jumba
na Mike Baraza.
Zanzibar; Mwadini Ally,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Nassor Masoud ‘Chollo’, Samir Hajji Nuhu, Aggrey
Morris Ambroce, Sabri Ally Makame, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Khamis Mcha
‘Vialli’, Jaku Juma Jaku/Abdallah Othman Ally, Amir Hamad Omar na Adeyom Saleh
Hemed/Seif Rashid Abdallah.