Yondan |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
BEKI wa
Tanzania Bara, Kevin Yondan ‘Vidic’ amesema hakupata maumivu makubwa jana
katika mchezo dhidi ya Somalia, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati,
CECAFA Tusker Challenge na anaamini baada ya kupumzika leo, kesho atakuwa fiti kucheza
dhidi ya Rwanda.
Bara,
Kilimanjaro Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, itashuka
dimbani kesho Uwanja wa Lugogo, kumenyana na Rwanda katika mchezo wa Robo
Fainali ya michuano hiyo iliyoanza Novemba 24 na inatarajiwa kutia nanga
Desemba 8 mjini hapa.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana Uwanja wa Lugogo baada ya mechi na Somalia, Yondan ambaye
pia marafiki zake humuita Cotton Juice, alisema aliumia kidogo kwenye goti la
mguu wa kulia kwa ndani, lakini baada ya mechi tu alianza kujisikia nafuu.
“Nadhani
kesho (leo) pia nikitumia tumia dawa, naamini pamoja na kupumzika nitakuwa fiti
kabisa kuendelea kucheza,”alisema beki huyo wa Yanga SC ya Dar es Salaam,
ambayo pia inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager.
Akiyazungumzia
mashindano kwa ujumla, Yondan alisema kwamba ni mazuri na mwaka huu timu nyingi
zimecheza kwa viwango vya hali ya juu.
“Hata hawa
Somalia, tumewafunga 7-0, lakini utaona hadi dakika ya mwisho walikuwa wanakuja
kwetu, na wao wamepoteza nafasi vile vile, kwa kweli mashindano ni mazuri na
yanatujenga kwa kiasi fulani,”alisema Yondan, aliyetua Yanga msimu huu akitokea
kwa mahasimu Simba SC.
Hata hivyo,
Yondan alisema ana matumaini Kombe litakwenda Tanzania kulingana na morali
iliyopo kwenye timu yao kwa sasa. “Mechi na Rwanda itakuwa ngumu, lakini kwa
nilivyowaona kama hali ya Uwanja itakuwa nzuri, tutawafunga,”alisema.
Yondan kwa
sasa ni mhilimili wa safu ya ulinzi ya Bara na Taifa Stars kwa ujumla na
anapokosekana pengo lake huonekana kwa uwazi kabisa.