Pongezi kwake kocha
Mholanzi wa Yanga, Ernie Brandts kuwapa nafasi wachezaji chipukizi aliowapandisha
kutoka kikosi cha pili, George Banda na Rehani Kibingu katika mchezo wa jana
dhidi ya Tusker, akiendelea hivi atawainua mapema, kwani nao wanaonyesha wanaweza
na wako tayari. Katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara, Yanga ilikuwa
ina makipa wawili wa kuaminika, Yaw Berko raia wa Ghana aliyeuzwa FC St. Eloi
Lupopo na Ally Mustafa ‘Barthez’ (PICHANI KULIA)ambaye amebaki kama kipa namba moja kwa sasa. Ukirejea
nyuma kidogo katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
Berko alidaka hadi Robo Fainali alipoumia na kumpisha Barthez ambaye alidaka
hadi timu ikawa bingwa. Kwa sasa Berko hayupo, kuelekea mzunguko wa pili wa
Ligi Kuu na hata Kombe la Kagame mwakani Kigali, Rwanda Yanga wanatakiwa
kuhakikisha wanakuwa tena na makipa wawili wa uhakika. Wengi walitarajia
kipindi hiki kipa Said Mohamed (PICHANI KUSHOTO)angeanza kutayarishwa na hata katika mchezo wa
jana dhidi ya Tusker alitarajiwa kudaka yeye, lakini ajabu akasimama Barthez
langoni.
Benchi la ufundi la
Yanga, lijiulize kama halitaanza wakati huu kumtayarisha Said ambaye tayari
Watanzania wanajua ni kipa mzuri, litafanya lini kazi hiyo? Mechi ya jana
ilikuwa ni nzuri Said kudaka kwa sababu Tusker ni timu nzuri na mabingwa wa
Kenya, lakini ajabu Barthez ameendelea kudaka hadi kwenye mechi mazoezi dhidi
ya timu za mchangani kama Kijitonyama Stars.
Au tuseme kipa huyo wa zamani
wa Majimaji haaminiki mbele ya benchi la ufundi la klabu hiyo, na kama ni hivyo
kipindi cha usajili cha dirisha dogo kimepita kwa nini hakuruhusiwa kuondoka na
klabu ikasajili kipa mwingine?
Siku Barthez akiumia
ghafla uwanjani na mapema katika mchezo mgumu na muhimu, Yanga wasitarajie
miujiza wakimuinua Said ghafla pia kwenda kuchukua nafasi. Wanatakiwa waanze
kumuandaa taratibu.
|