Kocha wa Uganda, Mscotland Bobby Williamson kichwa kinamuuma akifikiria Stars |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
WAKATI Nusu
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge
zinafanyika leo mjini hapa, umeibuka wasiwasi mkubwa wa upangwaji matokeo kwa
lengo la kuzikutanisha Kenya na Uganda katika fainali.
Kenya itaanza
kumenyana na Zanzibar saa 10:00 jioni na baadaye Uganda itamenyana na Tanzania
Bara saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, mjini hapa.
Habari za
kiuchunguzi ambazo zimefikia BIN ZUBEIRY, zimesema kwamba kwa
sababu mashindano haya hayakuwa na mahudhurio mazuri ya watu, maana yake CECAFA
na wenyeji FUFA wamepata hasara, wanataka kutafuta namna ya kupata fedha
angalau kidogo kwenye mechi ya mwisho.
Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye, kweli wamepanga matokeo? |
Na wanaamini
bila kuwapo mwenyeji kwenye fainali, mechi haitakuwa na mvuto kabisa mjini
hapa, hivyo inadaiwa kuna mpango maalum wa kuibeba Uganda iifunge Bara iingie
fainali.
Lakini pia
inaelezwa kutokana na upinzani na ujirani wa Kenya na Uganda, wenyeji wanaamini
fainali ikizikutanisha timu hizo itakuwa na mvuto- hivyo inadaiwa kuna maelekezo
maalum kwa marefa waibebe Harambee Stars dhidi ya Zanzibar Heroes.
Katibu wa
CECAFA, Mkenya Nicholas Musonye hajapatikana kuzungumzia shutuma hizo, lakini BIN
ZUBEIRY inaendelea kumtafuta ili kupata kauli yake juu ya hilo. Musonye
ameonyesha ukereketwa wa wazi katika mashindano haya pindi timu yake, Kenya
inapocheza mjini hapa, kwani inapokuwa inaelemewa huwa mnyonge sana.
Tayari kocha
wa Bara, Mdenmark Kim Poulsen ametoa tahadhari ya kuomba uchezeshwaji wa haki
katika mchezo wa leo jioni.
“Vijana
wamejiandaa vizuri kabisa na wote wako katika hali nzuri ya kucheza ila
tunachoomba ni uchezeshaji wa haki kutoka kwa refa, maana tunacheza na wenyeji
ambao wana watazamaji wengi,” alisema.
Poulsen alisema
timu zote mbili ni nzuri na iwapo muamuzi atachezesha vizuri basi utakuwa ni mchuano
mkali.
Mechi
zote zitaonyeshwa na Televisheni ya kulipia, SuperSport ya Afrika Kusini, ambapo
watazamaji watapata fursa nzuri ya kujionea mbivu na mbichi juu ya uchezeshaji
wa marefa. Mungu ibariki Tanzania. Amin.