Makocha wa Stars, Kim Poulsen na msaidizi wake Sylvester Marsh |
Na Mahmoud Zubeiry
TIMU ya
taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars iliyokuwa inashiriki michuano ya Kombe la
Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mjini Kampala, Uganda,
inarejea Dar es Salaam leo Jumapili baada ya kuambulia nafasi ya nne.
Stars
iliyotolewa katika Nusu Fainali na mabingwa mara mbili mfululizo, Uganda, The
Cranes kwa kuchapwa mabao 3-0, jana ilifungwa tena kwa penalti 6-5 na Zanzibar
katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu, Uwanja wa Mandela, Namboole mjini
Kampala kufuatia sare ya 1-1.
Timu hiyo
itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11:00 kamili
jioni kwa ndege ya PrecisionAir.
Baada ya
Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes kumaliza kushiriki mashindano ya Kombe la
Challenge mjini Kampala, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen kesho Jumatatu
(Desemba 10, 2012) saa 6 kamili mchana ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) atatangaza kikosi chake kitakachoingia kambini jioni ya Desemba
12, 2012 jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa
wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) itakayofanyika Desemba 22, 2012 katika Uwanja
wa Taifa.