Paul Were |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KATIKA kile
kinachoonekana kuwa ni mchecheto wa mechi dhidi ya Zanzibar, Kenya imeongeza wachezaji
wawili Paul Were na Kevin Omondi kwa ajili ya mechi hiyo ya Nusu Fainali ya
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge
inayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
Wawili hao
waliondoka jana usiku Nairobi, mara tu baada ya Harambee Stars kuvuzu Fainali,
wakiifunga 1-0 kwa mbinde Malawi na tayari wapo Kampala, Uganda kwa ajili ya
mchezo huo dhidi ya Zanzibar Stars.
Baada ya
kuifunga 1-0 Sudan Kusini katika mchezo wa pili wa Kundi A, wachezaji hao walikwenda
kujirusha kwenye klabu ya usiku na kurejea kambini na wanawake, jambo ambalo
lilifanya asubuhi yake waoandishwe ndege wote kurejea Nairobi, lakini kutokana
na mchecheto wa mechi ya kesho, wamerejeshwa.
Kocha wa Harambee
Stars, James Nandwa aliliomba Shirikisho la Soka Kenya (FKF) liliwarejeshe wachezaji
hao kwa ajili ya Nusu Fainali.
Kocha wa Fisa
FC, Charles ‘Korea’ Omondi, ambaye amekuwa akifanya mazoezi na wachezaji hao tangu
warejeshwe nyumbani, amethibitisha wamebadilika kinidhamu na wako vizuri
kimchezo.
Were na
Omondi wapo kwa mkopo AFC Leopards na Gor Mahia kutoka timu inayoshiriki Ligi
ya Jimbo la Nairobi, Fisa FC.
Mchezo kati
ya Zanzibar Heroes na Kenya utaanza kesho saa 10:00 jioni, ukifuatiwa na Nusu
Fainali ya pili, kati ya Uganda na Tanzania Bara Kilimanjaro Stars.