![]() |
Atudo |
Na Prince Akbar
BEKI
Joackins Atudo na kiungo Humphrey Mieno wote raia wa Kenya, wamewasili jana Dar
es Salaam kujiunga na klabu yao, Azam FC baada ya kumaliza kula sikukuu ya
Krisimasi na keshokutwa watakuwapo kwenye kikosi kitakachokwenda visiwani
Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Meneja Msaidizi
wa Azam, Jemedari Said ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mbali na
wachezaji hao wa Kenya, mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Brian Umony atatua
kesho.
Atudo na
Mieno walikuwepo kwenye kikosi cha Azam kilichotwaa Kombe la Hisani la Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka la
DRC wiki iliyopita, baada ya kuwachapa wenyeji, Dragons FC kwa penalti 4-2
kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Azam iliingia
fainali, baada ya kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya DRC
Ijumaa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs.
Kikosi kizima
cha Azam kilichoshiriki mashindano hayo ni Kipre Tchetche, Seif Abdallah, Kipre
Balou, Zahor Pazi, Jackson Wandwi, Malika Ndeule, Uhuru Suleiman, Omar Mtaki,
Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba, Abdi Kassim, Luckson Kakolaki,
Samih Hajji Nuhu, Mwadini Ally, Himid Mao, David Mwantika, Waziri Salum, Humphrey
Mieno na Joackins Atudo.
Katika
mashindano hayo, Gaudence Mwaikimba aliibuka mfungaji bora kwa mabao yake
matatu, ukiachilia mbali mawili ya penalti. Mchezaji mwingine wa kigeni wa
Azam, Brian Umony wa Uganda, atajiunga na timu hiyo baada ya sikukuu pia.
Azam
wamepangwa Kundi B, katika Kombe la Mapinduzi pamoja na Mtibwa Sugar ya Morogoro,
Coastal Union ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
Kundi A lina
timu za Simba SC, Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
Michuano ya Kombe
la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya
Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka
ndani na nje ya Tanzania.