Dhaira kulia akiwa na Hans Poppe baada ya kusaini miaka miwili Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA namba
moja wa Uganda, Abbel Dhaira mbali na kusaini mkataba wa miaka miwili wenye
thamani ya dola za Kimarekani 40,000, pia atakuwa akipokea mshahara wa Sh.
Mlioni 2 kwa mwezi.
Dhaira alisaini
mkataba jana katika hoteli ya JB Belmonte, Dar es Salaam mbele ya Katibu wa Simba,
Evodius Mtawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans
Poppe.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, baada ya kumsajili kipa huyo, Hans Poppe alisema kwamba
huyu ni kipa wa kwanza mwenye umbo kubwa tangu, kumalizika kwa zama za Mwameja
Mohamed katika klabu hiyo.
“Naamini
tumepata mtu sahihi na katika wakati mwafaka, hakuna asiyejua umahiri wa Dhaira
langoni, sasa tunasubiri kuvuna matunda ya kumsajili,”alisema Hans Poppe,
Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), ambaye leo anapanda
ndege kwenda Uingereza kwa mapumziko ya Krisimasi na mwaka mpya.
Hans Poppe aliyepigana
vita dhidi ya Uganda, alisema kwamba Dhaira ni kipa ambaye amependekezwa na
kipa wao wa kwanza hivi sasa, Juma Kaseja hivyo anaamini wawili hao wataishi vizuri
na kushirikiana.
Kwa upande
wake, Dhaira ambaye anarejea leo kwao Uganda kwenda kuchukua vifaa vyake vya
kazi kwa ajili ya kuja kuanza kumtumikia mwajiri wake mpya, alisema kwamba amefurahi
kusaini Simba SC na atafanya vizuri ili kuwafurahisha mashabiki wa klabu hiyo.
“Simba ni klabu
kubwa Afrika na inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika, kuna wachezaji rafiki zangu
na ndugu zangu, Mussa Mudde na Emmanuel Okwi, lakini Afrika Mashariki ni moja,
wachezaji wote wa Simba ni ndugu zangu, nitajisikia nipo nyumbani kabisa”alisema
Dhaira, anayetua Simba akitokea I.B.V FC ya Iceland.
Dhaira aliyeibukia
Express ya Uganda mwaka 2006, mwaka 2008 alihamia U.R.A. pia ya Uganda, ambayo
aliichezea hadi mwaka 2010 alipohamia Ulaya.
Kwa kumpata
Dhaira, Simba SC imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza,
Juma Kaseja ambaye amekuwa akisoteshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo
inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha
uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi
za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja
alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha
mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili
katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu
hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema
hataki tena kuchezea Simba.
Lakini
pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako
ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.