Dhaira |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC
imemalizana na kipa namba moja wa Uganda, Abbel Dhaira ambaye amemaliza mkataba
na klabu ya I.B.V FC ya Iceland na amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili
kwa dau ambalo halijafahamika.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY leo, Dhaira alisema kwamba amefikia makubaliano na Simba
kusaini mkataba wa miaka miwili kuja kuanza maisha mapya Dear es Salaam.
“Kila kitu
safi, nasubiri wanitumie tiketi niende Dar es Salaam kusaini,”alisema Dhaira.
Alipoulizwa Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe kuhusu mchezaji huyo,
alisema; “Kweli, atakuja kusaini wakati wowote hapa,”alisema Kapteni huyo wa
zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Dhaira
ambaye aliibukia Express ya hapa mwaka 2006 kabla ya 2008 kuhamia U.R.A. pia ya
hapa, ambayo aliichezea hadi 2010 alipohamia Ulaya atatua Dar es Salaam
Jumatatu kumaliza kila kitu Simba.
Kwa kumpata
Dhaira, Simba SC imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza,
Juma Kaseja ambaye amekuwa akisotoshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo
inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha
uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi
za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja
alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha
mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili
katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu
hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema
hataki tena kuchezea Simba.
Lakini
pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako
ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.
Awali Simba ilitaka kusajili kipa namba mbili wa Uganda, Hamza Muwonge, lakini baada ya kukubaliana na Dhaira, sasa imebadilisha mawazo.