Dhaira |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba, kipa namba
moja wa Uganda, Abbel Dhaira anatua leo Dar es Salaam kwa ajili ya kusaini
mkataba wa kuanza kuitumikia klabu hiyo.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) aliyepigana vita dhidi ya Uganda, alisema kwamba baada ya kumalizana na
kipa huyo, watahamia kwenye suala la mshambuliaji Brian Umony pia wa
Uganda.
Hata hivyo,
mapema juzi akizungumza na BIN ZUBEIRY, Dhaira alisema kwamba
anataka Simba wamtume mtu Kampala, Uganda na fedha ili asaini akiwa huko.
Dhaira alisema
kwamba hawezi kujihesabu kama tayari yeye ni kipa wa Simba hadi hapo
watakaposaini mkataba, kwani kwa sasa wamezungumza na kufikia makubaliano, ila
ikitokea timu nyingine ya kumaliza naye haraka, hatasita kufanya hivyo.
“Simba
wamezungumza na mimi ndio, lakini hatujamalizana, wao wakituma mtu kuja huku
tukasaini, hapo ndio nitakuwa nimejifunga, ila kwa sasa kama ipo timu nyingine
hata huko Tanzania inanitaka, milango bado iko wazi,”alisema Dhaira.
Dhaira
alisema kimsingi yeye yuko tayari kujiunga na Simba kwa kuwa ni klabu kubwa
Afrika na inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika na angependa kuungana na Mganda
mwenzake, Emmanuel Okwi huko.
Tayari Simba
SC imefikia makubaliano na kipa huyo namba moja wa Uganda, aliyemaliza mkataba wake
na klabu ya I.B.V FC ya Iceland na amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili
kwa dau ambalo halijafahamika.
Dhaira
alisema kwamba amefikia makubaliano na Simba kusaini mkataba wa miaka miwili
kuja kuanza maisha mapya Dear es Salaam.
Dhaira
ambaye aliibukia Express ya hapa mwaka 2006 kabla ya 2008 kuhamia U.R.A. pia ya
hapa, ambayo aliichezea hadi 2010 alipohamia Ulaya atatua Dar es Salaam
Jumatatu kumaliza kila kitu Simba.
Ikimpata
Dhaira, Simba SC itakuwa imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa
kwanza, Juma Kaseja ambaye amekuwa akisotoshwa peke yake bila kupumzika. Na
hiyo inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa
kuonyesha uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi
za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja
alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha
mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili
katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu
hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema
hataki tena kuchezea Simba.
Lakini
pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako
ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.