Dhaira anajitia kitanzi leo Msimbazi |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA namba
moja wa Uganda, Abbel Dhaira leo anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili
kwa ajili ya kuitumikia Simba baada ya kutua jana jioni mjini Dar es Salaam
akitokea kwao Uganda.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans
Poppe alisema kwamba, baada ya kusaini leo, Dhaira atarejea kwao mara moja kwa
ajili ya kwenda kujiandaa kuja kuanza kazi rasmi Msimbazi.
Kapteni huyo
wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) aliyepigana vita dhidi ya
Uganda, alisema kwamba Dhaira hatachelewa kurejea kuanza kumtumikia mwajiri
wake mpya, bali atakuja mapema.
Dhaira
amekwishasema atafurahi kujiunga na Simba kwa kuwa ni klabu kubwa Afrika na
inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika na angependa kuungana na Mganda mwenzake,
Emmanuel Okwi huko.
Tayari Simba
SC imefikia makubaliano na kipa huyo namba moja wa Uganda, aliyemaliza mkataba
wake na klabu ya I.B.V FC ya Iceland na amekubali kusaini mkataba wa miaka
miwili kwa dau ambalo halijafahamika.
Dhaira
alisema kwamba amefikia makubaliano na Simba kusaini mkataba wa miaka miwili
kuja kuanza maisha mapya Dear es Salaam.
Dhaira aliyeibukia
Express ya Uganda mwaka 2006, mwaka 2008 alihamia U.R.A. pia ya Uganda, ambayo
aliichezea hadi mwaka 2010 alipohamia Ulaya.
Ikimpata
Dhaira, Simba SC itakuwa imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa
kwanza, Juma Kaseja ambaye amekuwa akisotoshwa peke yake bila kupumzika. Na
hiyo inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa
kuonyesha uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi
za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja
alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha
mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili
katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu
hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema
hataki tena kuchezea Simba.
Lakini
pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako
ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.