Iddi Abubakar |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
KOCHA wa
makipa wa Azam, Iddi Abubakar Mwinchumu amesema kwamba, jana walilazimishwa
sare ya 1-1 na Dragons ya hapa katika mchezo wa Kundi B kuwania Kombe la Hisani
kwenye Martyrs mjini hapa kutokana na uchovu wa safari na pia timu kucheza bila
makocha wake.
Akizungumza
baada ya mechi ya jana mjini hapa, Iddi alisema kwamba timu ilifika usiku sana
wa juzi na jana ikaingia uwanjani, hivyo wachezaji walikuwa wana uchovu, lakini
anaamini mechi ijayo kesho watashinda.
Aidha, Iddi
alisema pia timu kucheza bila makocha wake, ambao wamebaki Kenya nako kwa namna
moja au nyingine kulichangia matokeo hayo. “Ilikuwa ghafla tu, nikaambiwa Iddi
utaongoza timu katika mechi hii, nashukuru tumepata sare na tumecheza mpira
mzuri sana kila mtu ameona, ila kama makocha wangekuwapo tungecheza vizuri
zaidi na tungeshinda,”alisma Iddi ambaye ni kocha wa makipa Azam na kipa wa zamani wa timu hiyo.
Azam
ilicheza mechi hiyo bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na
Msaidizi wake, Kali Ongala ambao wamebaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari
Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche kutokana na
kukosa viza za kuingia DRC.
Katika mechi
ya jana, hadi mapumziko, wenyeji walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani
na mshambuliaji wao hatari, Nkate Jason dakika ya 24.
Nkate
alifunga bao hilo baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Azam, ambao
walichanganyana na kipa wao, Mwadini Ally. Pamoja na kufungwa, Azam walicheza
vizuri katika dakika 45 za kwanza na zaidi walikosa mipango tu ya kumalizia.
Hata hivyo,
mashambulizi ya pembeni ya wapinzani wao yalilitia misukosuko ya kutosha lango
la Azam katika ngwe hiyo.
Kipindi cha
pili Azam walirudi na kikosi kile kile, lakini walibadilika kiuchezaji na
iliwachukua dakika nne tu kukomboa bao, kupitia kwa Nahodha mpya, Jabir Aziz
aliyeunganisha pasi ya Abdi Kassim ‘Babbi’.
Baada ya bao
hilo, Azam waliendelea kushambulia lango la wapinzani wao, lakini safu ya
ulinzi ya Dragons ilisimama imara kudhibiti mashmbulizi hayo.
Katika
dakika ya 76, kipa Mwadini alipangua kwa uhodari mkubwa mkwaju wa penalti wa
Mukinzi Mawesi, baaada ya mchezaji huyo huyo kuangushwa kwenye eneo la hatari
na Ibrahim Mwaipopo.
Baada ya
hapo Azam walihamia langoni mwa Dragons, ambao safu yao imara ya ulinzi
iliwanusuru adhabu hii leo.
Azam ambao
ni washindi wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame
na Ligi Kuu, wamepangwa katika Kundi B pamoja na Dragons na Shark FC, ambayo
watacheza nayo Desemba 17.
Ikifuzu
kwenye kundi lake, Azam itaingia Nusu Fainali moja kwa moja, ambazo zitachezwa
Desemba 25 na Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa
tatu.
Kundi B,
lina timu za DC Motema Pembe, Diables Noirs, FC MK na Real De Kinshasa.