Hans Poppe |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
SIMBA SC
imesema haitaki ugomvi wala malumbano na Azam FC, bali wanataka warudishwe
fedha zao zote walizotoa kumsaini mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa, Sh.
Milioni 55 pamoja na faida juu.
Azam FC jana
imemuuza Mrisho Khalfan Ngassa kwa dola za Kimarekani 75,000 (Sh. Milioni 120)
kwenda El Merreikh ya Sudan ambako amesaini mkataba wa miaka miwili,
utakaomuwezesha kulipwa mshahara wa dola za Kimarekani 4,000 (Sh Milioni 6,) kwa
mwezi huku naye akilipwa dola 50,000 (Sh. Milioni 75) za kusaini.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY kwa simu jana kutoka Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alisema kwamba wao walimsajili
mchezaji huyo kwa taratibu, ila wanashangaa sasa Azam wanataka kufanya mambo
kinyume cha utaratibu.
“Sisi tuna
mkataba na huyu mchezaji, ambao tulisaini na wao Azam, ambao ilikuwa kama
kuununua mkataba wake wa kule Azam, baada ya wao wenyewe kushindwana na huyo
mchezaji. Tuliwapa Sh. Milioni 25 na baadaye tukaongeza naye mchezaji mkataba
wa mwaka mmoja, tukampa Sh. Milioni 30,”alisema Hans Poppe.
Kapteni huyo
Mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema kwa kuwa hawataki
malumbano na Azam, wanaomba warejeshewe fedha zao na faida kidogo, kwani
mchezaji huyo amenunuliwa akiwa anachezea Simba SC.
Awali,
Merreikh walitaka kumpa mkataba wa miaka mitatu Ngassa wenye thamani ya dola
100,000, lakini wakala wake Alhaj Yussuf Said Bakhresa akakataa akisema
utambana mchezaji wake aking’ara na kutakiwa na klabu nyingine.
Sasa, Ngassa
baada ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge
mwishoni mwa wiki hii, atakwenda Sudan kufanyiwa vipimo tayari kujiunga na
klabu hiyo, ambayo ni jambo la kawaida kucheza hatua ya makundi ya michuano ya
klabu Afrika.
Azam
walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na
kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika
Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi
ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya
hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam
kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara
nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa
kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye
Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam
FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati
ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.