Na Mahmoud Bin Zubeiry |
MICHUANO ya
vijana chini ya umri wa miaka 20 ya klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
maarufu kama Kombe la Uhai, inatarajiwa kufikia tamati leo kwa mchezo wa
fainali kati ya Coastal Union ya Tanga na Azam kwenye Uwanja wa Karume, Dar es
Salaam.
Timu hizo
zimepata fursa hiyo baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali ya michuano
hiyo inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za
Ligi Kuu ya Vodacom jana. Michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim
Bakhresa kupitia maji Uhai.
Azam ndiyo
iliyokuwa ya kwanza kupata tiketi ya fainali baada ya kuitoa Mtibwa Sugar ya
Morogoro kwa mikwaju ya penalti 3-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90,
wakati Coastal Union iliivua ubingwa Simba kwa kuifunga mabao 2-1.
Mechi ya fainali
itaanza saa 10 kamili jioni, na itatanguliwa na ile ya kutafuta mshindi wa tatu
kati ya Mtibwa Sugar na Simba ambayo itachezwa saa 2 kamili asubuhi kwenye
uwanja huo huo.
Mbali ya
kombe, bingwa wa michuano hiyo atapata sh. milioni 1.5, makamu bingwa sh.
milioni 1 wakati mshindi wa tatu atajinyakulia sh. 500,000. Timu iliyoonesha
zaidi mchezo wa kiungwana (fair play) itapata sh. 400,000, mchezaji bora wa
mashindano sh. 350,000, mfungaji bora sh. 300,000 na kipa bora sh. 300,000.
Naye kocha
bora katika mashindano hayo atazawadiwa sh. 300,000 kama itakavyokuwa kwa refa
bora.
Rais wa
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Sepp Blatter alikwishasema lengo ya wao
kutilia mkazo na kuimarisha mashindano ya vijana ni kuandaa nyota wa baadaye wa
soka.
Na unaweza
kuona nyota wengi wanaowika katika soka duniani hivi sasa, wametokea katika
mashindano hayo ya vijana.
John Michael
Nchekwube Obinna ama Mikel John Obi au John Obi Mikel wa Nigeria aliibukia
kwenye michuano ya U17 ya dunia mwaka 2003 iliyofanyika katika miji ya
Helsinki, Tampere, Lahti na Turku nchini Finland.
Japokuwa
Nigeria haikufua dafu kwenye Kundi lake B, lililokuwa na timu za Argentina
iliyoongoza kwa pointi zake tisa, Costa Rica iliyofuatia kwa pointi zake nne
sawa na Nigeria na kuzidiwa kwa wastani wa mabao tu, lakini soka nzuri ya Obi
ilimuuza na sasa mchezaji mkubwa Ulaya.
Hajatwaa
tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika, ndiyo- lakini ana Medali ya dhahabu ya Ligi
ya Mabingwa Ulaya na anachezea klabu kubwa, analipwa vizuri. Ni tajiri kutokana
na soka.
Lionel Andres
Messi au ‘Leo Messi’ aling’ara katika Kombe la Dunia la U20 mwaka 2005 nchini
Uholanzi, akiiwezesha Argentina kuwa bingwa naye akishinda tuzo za Mchezaji
Bora wa mashindano na mfungaji bora wa fainali hizo pia.
Leo huyu
bila kujiumauma dunia inakiri ndiye mchezaji bora zaidi mwenye kipaji cha kipekee,
ambaye akiwa ametia kibindoni tuzo tatu za Mwanasoka Bora wa Dunia, bado jibu
linakuwa gumu kama si yeye tuzo ya mwaka huu apewe nani mwingine?
Kwa ujumla
michuano ya vijana ni muhimu mno kumuandaa mchezaji bora wa baadaye, wataalamu
wanasema ki professional, hatua kwa hatua U17, U20, U23 na baada ya hapo
anakuwa mchezaji kamili, mwenye kustahili kuitwa senior.
Lakini ajabu
imetokea desturi mbaya sana katika mashindano ya vijana hapa Tanzania, timu
zinaingiza wachezaji waliozidi umri katika mashindano.
Desturi hii
wanayo sana watu wa Afrika Magharibi na imekwishawaumbua sana kwa wachezaji
kugundulika wamedanganya umri na hilo limepunguza soko la wachezaji wa Nigeria
duniani.
Tukienda
kwenye dhana halisi ya mashindano ya vijana, ambayo ni kumuandaa mchezaji wa
kesho, dhahiri ni kupoteza muda na kujidanganya wenyewe kwa kutumia wachezaji
waliozidi umri kwenye mashindano.
Tazama Kombe
la Uhai mwaka huu, imeshuhudiwa wachezaji wanarudi kwa mara ya nne katika
vikosi vyao, eti bado U20 na ukitazama hata mwonekano wao, dhahiri unapata
picha ya udanganyifu.
Bodi za soka
haziwezi kusimamia kila kitu au kuwa na wepesi wa kugundua kila kitu cha uongo,
ikiwa wanaodanganya wanakuwa wamejipanga kuhalalisha uongo wao.
Lakini
pamoja na yote, kuna kiwango ambacho anafikia mchezaji na baada ya hapo hupaswi
kumrudisha chini, bali anatakiwa kuendelea kukomazwa na kujengwa zaidi huko
juu, ili kutoa nafasi ya kuandaa vijana wengine.
Ramadhani
Singano, Edward Christopher wote ni hawa ni wachezaji wa kikosi cha kwanza cha
Simba na timu ya taifa, Taifa Stars- kuwarudisha chini ni kuwarudisha nyuma wao
wenyewe, bila hata kuangalia umri wao.
Au Simon
Msuva na Frank Domayo, wote hawa ni wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Yanga na
timu ya taifa, hawapaswi kurudishwa chini na ndiyo maana Samuel Eto’o tangu
aweke rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kucheza Fainali za Kombe la Dunia
Juni 17, mwaka 1998, hakuwahi kurudishwa chini, zaidi tu ya kuchezea kikosi cha
Olimpiki mwaka 2000 kilichoshinda Medali ya Dhahabu.
Akiwa na
umri wa miaka 17 na miezi mitatu, Eto’o aliichezea Cameroon nchini Ufaransa
ikilambwa 3–0 na Italia katika hatua ya makundi na baada ya hapo akawa mchezaji
wa kudumu wa kikosi cha wakubwa cha Simba Wasiofungika.
Sababu ya
FIFA kuamua kuleta vipimo vya kubaini umri halisi wa wachezaji ni kutokana na
kuona dhana yao ya mashindano ya vijana inapotoshwa- watu wamekuwa wagumu
kuelewa na ndiyo maana ukifuatilia wachezaji wa Afrika miaka ya karibuni
wanaibuka na kupotea baada ya mfupi.
Siku moja
Tanzania tukiamua kufuata misingi halisi ya soka na miiko yake, tutafanikiwa,
lakini kama tutaendelea na usanii wetu, basi tutaendelea kuwa watu wa
kubahatisha bahatisha tu na hatutafika popote.
Sasa tuamue
kutumia vema mashindano ya vijana kwa kutumia wachezaji wanaostahili au
kuendelea kuweka vijeba kwa tamaa ya kutwaa ubingwa, lakini mwisho wa siku
hatujengi?
Tunajidanganya,
tunawapotezea muda wachezaji na mwisho wa siku watadumaa bila kufika popote.
Ndiyo, kuwafanya wao watoto siku zote ni kuwadumaza hata kiakili. Wasalam!