Na Princess Asia
SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF) linaupongeza uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu wa
Wanawake Tanzania (TWFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana
(Desemba 19 mwaka huu) hoteli ya Midlands mjini Morogoro.
Ushindi
aliopata Lina Kessy aliyechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe
wengine wa Kamati ya Utendaji unaonesha jinsi ambavyo wajumbe wa Mkutano Mkuu
wa TWFA walivyo na imani kwao.
TFF inaahidi
kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TWFA, na kwamba ina
changamoto kubwa ya kuhakikisha inaendesha shughuli za chama hicho kwa
kuzingatia katiba na kanuni.
Pia tunatoa
pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini ya Mama Ombeni Zavala na Kamati ya
Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Deogratias Lyatto kwa kuhakikisha uchaguzi huo
unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia Katiba ya TWFA na Kanuni za Uchaguzi
za Wanachama wa TFF.
Safu mpya ya
uongozi wa DRFA inaundwa na Lina Kessy (Mwenyekiti), Rose Kissiwa (Makamu
Mwenyekiti), Amina Karuma (Katibu), Zena Chande (Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa
TFF) wakati mjumbe wa Kamati ya Utendaji ni Triphonia Temba.