TENGA
AWASHUKURU WALIOPIGIA KURA WARAKA
Rais wa TFF, Tenga |
Na Boniface Wambura
RAIS wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewashukuru Wajumbe wa
Mkutano Mkuu kwa kupigia kura waraka wa marekebisho ya Katiba, kwani wametimiza
wajibu wao.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo, Rais Tenga amesema marekebisho ya
Katiba ni jambo muhimu, lakini lazima yapate ridhaa ya wanaohusika ambao ni
wajumbe.
“Nawasukuru
wajumbe kwa kupitisha jambo hili. Nawashukuru wote, waliokubali na waliokataa.
Ndivyo demokrasia ilivyo. Tulitaka waseme ndiyo au hapana, hivyo tulitarajia
kupata majibu yoyote kati ya hayo mawili.
Marekebisho
mengine yalikuwa ni maelekezo (directives) kutoka FIFA na CAF. Katiba yetu
inasema tutatekeleza maagizo ya CAF na FIFA, lakini kwa misingi ya utawala bora
tuliona ni lazima tupate ridhaa kutoka kwa wajumbe,” amesema.
Jumla ya Wajumbe
waliopiga kura kwa njia hiyo ya waraka ni 103 ambapo 70 waliunga mkono wakati
waliokataa ni 33. Idadi hiyo ni asilimia 68 ya kura zote zilizopigwa, hivyo
kupatikana theluthi mbili ya kura zilizopigwa ili kufanya marekebisho kikatiba.
Vipengele
vilivyoingizwa katika marekebisho hayo ni ‘club licencing’ kama ilivyoagizwa na
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF kama
ilivyoshauriwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na kuondoa
nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Vilevile
Kamati ya Utendaji itakutana Desemba 23 mwaka huu kufanya marekebisho ya Kanuni
za Uchaguzi, kutokana na kupitishwa kwa marekebisho hayo ambayo yanaunda Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF. Pia itachagua wajumbe wa Kamati ya Rufani ya TFF.
Mkutano Mkuu
wa TFF ambapo pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi utafanyika Februari 23 na 24
mwakani. Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wajumbe wanatakiwa kupewa taarifa ya
Mkutano Mkuu siku 60 kabla. (Mwandishi wa Habari hizi ni Ofisa Habari wa
TFF)