Patrick Liewig |
Na Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. ambaye awali ilielezwa atatemwa
kwenye kikosi cha Simba SC, amerejeshwa kwenye kikosi hicho.
Sunzu |
Katibu wa
Simba SC, Evodius Mtawala ameiambia BIN ZUBEIRY Sunzu ameomba mwenyewe
kurudi kazini na tayari amekwishawasili Dar es Salaam na ameanza mazoezi.
“Kama
utatakumbuka lilikuwa suala la kiafya, Sunzu alikuwa mgonjwa akaomba aachwe,
lakini nadhani baada ya kurejea kwao na kutibiwa ameona amepona na ameomba
kurudi kazini,”alisema Mtawala.
Mtawala
alisema Sunzu ni miongoni mwa wachezaji waliotarajiwa kuondoka jana mjini Dar
es Salaam kwenda visiwani Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi. Aidha, Mtawala
pia alisema mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa pia ameungana na wenzake
mazoezini tangu jana.
Wakati huo
huo, kocha mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig aliyewasili jana mchana Dar
es Salaam, leo anatarajiwa kusaini mkataba wa kuanza kazi Msimbazi.
Mtawala
alisema, Liewig atakaposaini mkataba atakwenda kuungana na kikosi cha Wekundu
hao wa Msimbazi visiwani Zanzibar tayari kuanza kazi.
Liewig
ambaye ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa,
ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, jana usiku
alitambulishwa mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba katika hoteli ya
Spice.
Liewig
mwenye Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya
vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller, anatarajiwa
kwenda Zanzibar kesho.
Liewig pia
amehudhuria kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo
Kikuu cha Dijon.
Kwa upande
wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha
Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za
timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha
kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia
mwaka 1989 hadi 1990: alikuwa Meneja
Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi
1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez,
1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa
Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia
alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa
ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari
mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za
U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia
mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa
mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super
Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya
makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa
Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba
mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia.