Stewart wa kwanza kushoto akifutiwa na Kali, Kocha wa Makipa Iddi Abubakar na Daktari, Paulo Gomez raia wa Ujerumani |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
KOCHA Mkuu
wa Azam FC, Stewart Hall ameondoka jana usiku mjini hapa kwenda kwao Uingereza
kwa ajili ya sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya, akiiacha timu inakabiliwa na
mchezo wa fainali ya Kombe la Hisani hapa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akizungumza na
BIN
ZUBEIRY kabla ya kuondoka mjini hapa, Stewart alisema kwamba anamuachia
timu hiyo msaidizi wake, Kali Ongala na anaamini atafanya kazi nzuri.
Stewart alisema
Kali ni mtu ambaye siku zote amekuwa akimuandaa kuwa kocha wa baadaye wa Azam na
hii si mara ya kwanza kumuachia timu, kwani aliwahi kufanya hivyo mara kadhaa
ikiwemo kwenye Kombe la Urafiki, ambalo aliiongoza timu kufika Fainali.
“Siku moja
nitaondoka Azam na kumuacha Kali awe kocha Mkuu, siku zote namtayarisha,
namjengea kujiamini, naamini atakuwa kocha bora sana wa Azam, sina wasiwasi
naye, namuachia timu na anaweza kurudisha Kombe Dar es Salaam,”alisema Stewart
ambaye atarejea mwakani.
Azam kesho
itacheza fainali, baada ya jana kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4
Shark FC ya hapa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa
Martyrs.
Nahodha
Jabir Aziz Stima ndiye aliyekwenda kupiga penalti ya mwisho, Shark wakitoka
kupoteza, kufuatia mpira kugonga mwamba. Aiziz aliwainua vitini wachezaji
wenzake na makocha wake pamoja na viongozi wa wachache wa timu hiyo waliopo
hapa kwa kupiga penalti maridadi iliyotinga nyavuni.
Azam
iliuanza mchezo huo vizuri na ikicheza kwa maelewano makubwa sambamba na
kushambulia kwa kasi kutokea pembeni, kulia Kipre Herman Tchetche na kushoto
Seif Abdallah.
Hata hivyo, shambulizi
la kushitukiza la Shark liliwapa bao la kuongoza dakika ya 16, lililofungwa na
Ngulubi Kilua, baada ya mabeki wa Azam kudhani ameotea.
Iliwachukua
dakika 10 tu Azam kusawazisha bao hilo, mfungaji akiwa Gaudence Exavery
Mwaikimba aliyeunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya nyota wa mchezo huo,
Kipere Herman Tcheche kutoka wingi ya kulia.
Baada ya bao
hilo, Azam iliendelea kuwashambulia Shark na dakika ya 37, Kipre Tchetche
aliifungia timu hiyo bao la pili, kufuatia kazi nzuri ya Mwaikimba. Mwaikimba
alipokea mpira mrefu, akatuliza na kumtangulizia kwa mbele mfungaji, ambaye
hakufanya makosa, alimchambua kipa wa timu inayomilikiwa na mdogo wa rais wa
DRC, Joseph Kabila.
Hadi
mapumziko, Azam ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1 na kipindi cha pili Shark
waliingia kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha kwa penalti dakika ya 47,
iliyotiwa nyavuni na Bukasa Kalambai, ambaye yeye mwenyewe alijiangusha kwenye
eneo la hatari baada ya kuzongwa na beki David Mwantika.
Baada ya
dakika 90 kutimu timu hizo zikiwa zimefungana 2-2, sheria ya matuta ilichukua
mkondo wake na wachezaji wote watano wa Azam waliopewa dhamana hiyo na kocha
Muingereza Stewart Hall, walitimiza wajibu wao vizuri.
Kipre
Tchetche alifunga ya kwanza, Mwaikimba ya pili, Jaockins Atudo ya tatu, Himid
Mao ya nne na Stima akapiga ya ushindi.