Shujaa wa Stars leo, Ngassa (Picha ya Maktaba) |
Na Prince Akbar
KAMA ingekuwa
ni ndondi, leo Tanzania wangetawazwa kuwa mabingwa wapya wa Afrika, baada ya
kuwapiga Zambia, lakini katika soka, haiku hivyo.
Tanzania,
Taifa Stars leo imeendeleza wimbi lake la ushindi katika michezo ya kirafiki
baada ya kuifunga Zambia 1-0, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo
wa leo, hadi mapumziko, tayari Stars ambayo Novemba 14, mwaka huu iliifunga 1-0
Kenya, Uwanja wa CCM Kirumba, walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na
kiungo mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa.
Ngassa,
anayecheza kwa mkopo Simba SC akitokea Azam FC, zote za Dar es Salaam, alifunga
bao hilo dakika ya 45, akimalizia pasi nzuri ya kiungo wa Simba SC, Mwinyi
Kazimoto.
Stars ilicheza
vizuri na kwa umakini wa hali ya juu kipindi cha kwanza, na kufanikiwa kuwabana
mabingwa hao wa Afrika wanaojiandaa kwenda kutetea taji lao nchini Afrika
Kusini mapema mwakani.
Kipindi cha
pili, Zambia walianza kwa kurekebisha kikosi chao, kocha Mfaransa, Herve Renard
akiwatoa Hichani Himonde, Moses Phiri, Sinkala na Isaac Chansa na nafasi zao
kuchukuliwa na Stopila Sunzu, Mukuka Mulenga, Evans Kangwa na Francis Kasonde.
Pamoja na
mabadiliko hayo, Stars iliendelea kung’ara na katika dakika ya 57 Ngassa
alikaribia kufunga tena kama si shuti lake kufuatia pasi ‘tamu sana’ ya Sure
Boy kutoka nje.
Lakini kukosa
kwa Ngassa bao hilo, kulitokana na maarifa ya beki wa TP Mazembe ya DRC,
Stopila Sunzu anayejiandaa kuhamia Reading ya England, ambaye alimbana kiungo
huyo wa Simba kumynima mwanya wa kupiga vizuri na akafanikiwa kumfanya apige
nje.
Zambia walipoteza
nafasi nzuri ya kusawazisha bao dakika ya 76, baada ya shuti la Chasamba Lungu
kugonga mwamba, wakati kipa Juma Kaseja akiwa amekwishapotea maboya.
Ngassa alijibu
shambulizi hilo dakika ya 77 baada ya shuti alilojaribu kupaa juu ya lango,
huku Felix Katongo akipewa kadi ya njano, baada ya kumuangusha Amri Kiemba
aliyekuwa anamfunga tela.
Juma Kaseja
alifanya kazi ya ziada dakika ya 86, baada ya kuokoa shuti la karibu la Chris Katongo
na katika dakika ya 87, Stars ilipata pigo baada ya beki Kevin Yondan kuumia na
nafasi yake kuchukuliwa beki mwenzake wa Yanga, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’
dakika ya 88.
Kikosi cha Stars
leo kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Kevin Yondan/Nadir
Haroub dk 87, Frank Domayo, Salum Abubakar, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba,
Mrisho Ngassa/Amir Maftah dk83 na Khamis Mcha ‘Vialli’/Simon Msuva dk59.
Zambia;
Danny Munyao, Chintu Kampamba, Hichani Himonde, Chisamba Lungu, James Chamanga,
Moses Phiri, Chris Katongo, Felix Katongom Nathan Sinkala/, Rodrick Kabwe na
Isaac Chansa.