Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
TANZANIA
Bara, Kilimanjaro Stars leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole
mjini hapa kumenyana na wenyeji, Uganda, The Cranes katika Nusu Fainali ya
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kuanzia
saa 12:00 jioni.
Mchezo huo,
utatanguliwa na mechi nyingine ya hatua hiyo kati ya Zanzibar na Kenya, ambayo,
itaanza saa 10:00 jioni.
Hii inakuwa
mara ya pili mfululizo, Bara kukutana na Uganda katika Nusu Fainali ya michuano
hii, kwani hata mwaka jana pia mjini Dar es Salaam, zilikutana katika hatua
hiyo, Desemba 8, Uwanja wa Taifa.
Katika
mchezo huo, wenyeji wakiwa chini ya makocha wazalendo, walichapwa mabao 3-1
ndani ya dakika 120, Stars ikitangulia kupata bao mapema tu dakika ya 18,
mfungaji Mrisho Khalfan Ngassa, lakini Nahodha wa The Cranes Andy Mwesigwa akasawazisha dakika ya 56.
Mchezo
ulipohamia katika dakika za nyongeza, Uganda walipata mabao mawili na
kuwamaliza wenyeji, wafungaji Emmanuel Okwi dakika ya 102 na Isaac Isinde dakika
ya 111 kwa penalti.
Kocha wa
Stars, Mdenmark Kim Poulsen ametahadharisha wanataka uchezeshaji wa haki kutoka
kwa refa Mohamed El Fadil wa Sudan, ambaye pia aliwachezesha katika mechi dhidi
ya Rwanda Robo Fainali.
“Vijana
wamejiandaa vizuri kabisa na wote wako katika hali nzuri ya kucheza ila
tunachoomba ni uchezeshaji wa haki kutoka kwa refa, maana tunacheza na wenyeji
ambao wana watazamaji wengi,” alisema.
Poulsen alisema
timu zote mbili ni nzuri na iwapo muamuzi atachezesha vizuri basi utakuwa ni mchuano
mkali. “Vijana wana ari na mchezo huu na tukipewa haki tutacheza vizuri kama
tulivyofanya katika michezo dhidi ya Rwanda,” alisema Poulsen.
Kuhusu hali
ya timu, Mdenmark huyo alisema hana majeruhi hata mmoja na pia aliwasifu
wachezaji wake kwa kuonyesha umoja na nidahmmu ya hali ya juu. “Hawa wanakaa
kama familia, si unawaona walivyo pamoja?” alisema Poulsen na kuongeza kuwa
hilo ni muhimu sana kwa mchezaji.
Kwa upande
wake, Kocha Msaidizi wa Stars, Sylvester Marsh amesema kama Uganda waliwafunga
Tanzania Dar es Salaam mwaka jana, basi na wao watawafunga Kampala mwaka huu.
Kocha wa
Uganda, The Cranes, Msoctland, Bobby Williamson alisema kwamba Stars ni timu
nzuri, lakini haina uwezo wa kuifunga timu yake.
“Wana
wachezaji wazuri, wenye vipaji, lakini bado timu yangu ni nzuri katika
mashindano haya, tutawafunga,”alisema.
Safu ya
ushambuliaji ya Stars leo inatarajiwa kuongozwa na Mrisho Khalfan Ngassa na
John Raphael Bocco ‘Adebayor’ ambao wanaongoza kwa mabao katika mashindano
haya, kila mmoja akiwa na mabao matano.
Uimara zaidi
wa Stars upo katika safu ya kiungo, ambako kuna watu mahiri kama Frank Domayo,
Amri Kiemba, Salum Abubakar na Mwinyi Kazimoto.
Stars pia
inajivunia safu imara ya ulinzi, chini ya Nahodha, kipa Juma Kaseja, mabeki
Erasto Nyoni, Amir Maftah, Kevin Yondan na Shomary Kapombe ambao wameruhusu bao
moja tu katika mechi nne zilizopita, tena la penalti, dhidi ya Burundi.
Bocco,
aliyeimarika zaidi kiuchezaji, mwenye nguvu, anayeenda hewani na kuambaa vema
na mpira, atasimama mbele ya mdomo wa goli la Korongo wa Kampala, wakati Ngassa
atakuwa akishambulia kutokea pembeni.
Domayo,
Kiemba na Sure Boy watakuwa wote wakikaba kwa bidii, wakati Kazimoto atakuwa
akiiendesha timu, zaidi ya kuwatengenezea nafasi za kufunga Bocco na Ngassa.
Kiemba amekuwa
akitumia mwanya wa timu kufanya mashambulizi ya kushitukiza kupanda kusaidia na
ndiyo maana aliwafunga Rwanda, jambo ambalo linatarajiwa na leo pia.
Kazimoto
mwenye mashuti makali hajafunga hata bao moja katika mechi nne zilizopita,
lakini matarajio ya wengi atatikisa nyavu kuanzia leo baada ya kuizoea zaidi
hali ya Kampala.
Uganda nao
wana ukuta sugu, ambao haujaruhusu hata bao moja hadi sasa, ikiongozwa na kipa
Hamza Muwonge, mabeki Iguma Dennis, Godfrey Walusimbi,Henry kalungi na Isaac
isinde, wakati safu ya kiungo ya kiungo inatarajiwa kuongozwa na Hassan Wasswa,
Geoffrey Kizito na Moses Oloya.
Safu ya
ushambuliaji leo bila shaka dhamana watapewa, Robert Ssentongo, Hamisi Kiiza na
Brian Umony, wakati Emmanuel Okwi anaweza kuanzia benchi tena. Mchezo wa leo
unatarajiwa kuwa mkali, Uganda wakicheza mbele ya malefu ya mashabiki wao na
Bara wakijaribu kulipa cha Dar es Salaam
mwaka jana.
Timu hizi
zimekutana mara 12 katika Challenge tangu mwaka 1975, kila timu ikishinda mechi
tano, sare mbili na Bara imefunga mabao 16, wakati imefungwa mabao 17.
Uganda; Hamza Muwonge, Iguma Dennis, Godfrey
Walusimbi, Henry Kalungi, Isaac Isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey Kizito, Moses
Oloya, Robert Ssentongo, Hamisi Kiiza na Brian Umony.
Tanzania; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir
Maftah, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Franko Domayo, Amri Kiemba, Salum
Abubakar, Mwinyi Kazimoto, John Bocco na Mrisho Ngassa.
Mungu
zibariki timu zetu, Bara na Zanziabr leo, ibariki Tanzania. Amin.
MATOKEO YA JUMLA STARS NA CRANES
TANGU 1975:
P W D L GF
GA Pts
Uganda 12 5 2 5 17 16 17
Tanzania 12 5 2 5 16 17 17
REKODI YA STARS NA CRANES CHALLENGE
TANGU 1974:
Desemba 8, 2011; Nusu Fainali, Dar es Salaam
Uganda 3–1
Tanzania (dakika 120)
Januari 9, 2009; Kundi A Uganda
Tanzania 1-2
Uganda
Desemba 11, 2001; Kundi B Rwanda
Tanzania 1-0
Uganda
Desemba 1, 1995; Kundi B Uganda
Tanzania 2-1
Uganda B
Desemba 10, 1994; Fainali Kenya
Tanzania 2-2
Uganda: (Tanzania ilishinda kwa penalti 4-3)
Desemba 10, 1992; Fainali Mwanza
Tanzania B(Kakakuona)
0-1 Uganda
Desemba 17, 1990; Nusu Fainali Zanzibar
Tanzania 1-1
Uganda (dakika 120, Uganda ilishinda penalti 6-5)
Desemba 1, 1984; Kundi A Uganda
Tanzania 1-1
Uganda
Novemba 20, 1983; Kundi A Kenya
Tanzania 1-1
Uganda
Novemba 17, 1982; Kundi A Uganda
Tanzania 0-1
Uganda
Novemba 9, 1979; Kundi A Kenya
Tanzania 5-3
Uganda
Desemba 10, 1974; Fainali Dar es Salaam
Tanzania 1-1
Uganda (Tanzania ilishinda kwa penalti 5-3)