Ssentongo |
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
MABAO mawili
aliyofunga mshambuliaji wa Uganda jana, Robert Ssentongo katika Nusu Fainali ya
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, yamemfanya
atimize mabao manne na sasa anazidiwa bao moja tu washambuliaji wawili wa
Tanzania, John Bocco na Mrisho Ngassa.
Hata hivyo,
mchuano wa watatu hao utafikia kilele kesho, wakati wote watakapopata mechi
moja moja za ziada kuboresha akaunti zao.
Uganda
itamenyana na Kenya katika fainali na Ssentongo atakuwa na nafasi nyingine ya
kufunga, wakati Bara itamenyana na Zanzibar na Ngassa na Bocco pia watakuwa
nafasi ya kuongeza mabao.
Ssentongo
jana aliiongoza Uganda kuzima ndoto za Bara kurejea nyumbani na Kombe la
Challenge baada ya kufungwa na wenyeji, The Cranes mabao 3-0 kwenye Uwanja wa
Mandela, Namboole mjini hapa.
Kwa matokeo
hayo, Uganda itamenyana na majirani zao na wapinzani wao wakubwa, Kenya katika
fainali Jumamosi, ambao katika mchezo wa kwanza waliitoa kwa mikwaju ya penalti
4-2 Zanzibar, kufuatia sare ya jumla ya 2-2 ndani ya dakika 120.
Zanzibar na
Bara zitamenyana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu siku hiyo hiyo ya
Jumamosi kwenye Uwanja wa Namboole.
Hadi
mapumziko, Uganda walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Emmanuel
Okwi dakika ya 11, baada ta kuuwahi mpira mrefu uliopigwa na kipa wake, Hamza
Muwonge na kufumua shuti kali la umbali wa mita 19, ambalo lilimshinda kipa
Juma Kaseja.
Baada ya bao
hilo, Okwi aliumia na kutoka nje dakika ya 36 nafasi yake ikichukuliwa na
Hamisi Kiiza.
Uganda ndio
waliouanza mchezo huo kwa kasi na kulitia misukosuko lango la Stars kwa
takriban dakika 10 mfululizo, lakini baada ya hapo timu hizo zikaanza
kushambuliana kwa zamu.
Timu zote
zilikuwa zikishambulia kutokea pembeni, lakini Uganda ndio walioonekana kuzalisha
mashambulizi ya hatari zaidi.
Kipa na
Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alitoka uwanjani baada ya dakika 45 za kipindi
cha kwanza akilaumiana na mabeki wake kwa kufungwa bao la kutanguliwa.
Kipindi cha
pili, Waganda walirudi na moto wao tena na kufanikiwa na kupata bao la pili
dakika ya 51, safari hii Robert Ssentongo akimtungua Kaseja, baada ya mabeki wa
Stars kudhani ameotea.
Pamoja na
kufungwa bao la pili, Stars waliendelea kucheza kwa juhudi, ingawa Waganda
waliendelea kutawala mchezo.
Mpira uliotemwa
na Juma Kaseja kufuatia shuti la Moses Oloya, ulimkuta Ssentongo dakika ya 71
akaukwamisha nyavuni na kuipatia The Cranes bao la tatu. Kutoka hapo, hali
ilikuwa mbaya kwa Stars.
Zikiwa
zimesalia dakika tano mchezo kumalizika, taa za Uwanja wa Mandela zilizimika,
lakini baada ya jitihada za pamoja za FUFA, CECAFA na uongozi wa Uwanja,
ziliwaka baada ya dakika saba na mchezo kuendelea hadi filimbi ya mwisho.
WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE
2012
John Bocco Tanzania 5
Mrisho
Ngassa Tanzania 5
Robert
Ssentongo Uganda 4
Brian Umony Uganda 3
Khamis Mcha Zanzibar 3
Suleiman
Ndikumana Burundi 3 (1 penalti)
Chris
Nduwarugira Burundi 3
Geoffrey
Kizito Uganda 2
David
Ochieng Kenya 2
Clifton
Miheso Kenya 2
Dadi Birori Rwanda 2
Mike Barasa Kenya 2