Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
WEKUNDU wa
Msimbazi, wako mbioni kusajili wachezaji wawili wa timu ya taifa ya Uganda, The
Cranes, kipa Hamza Muwonge na mshambuliaji Brian Umony, ingawa suala la kocha
wa Malawi, Kinnah Phiri halijakaa vizuri bado.
BIN ZUBEIRY jana ilishuhudia mazungumzo kati ya
Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili
ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe na mshambuliaji huyo wa zamani wa SuperSport
United ya Afrika Kusini kwenye hoteli ya Sheraton mjini hapa.
Hata hivyo,
baada ya mazungumzo hayo jana, Simba iliomba mchezaji huyo awasiliane nao leo,
ili kwanza watafakari yale anayoyataka.
Kwa ujumla
Simba imeridhia kumpa Umony anachokitaka na bila shaka leo watamalizana. Wakati
huo huo, Simba inataka kufanya mazungumzo na kipa namba mbili wa Uganda, Hamza
Muwonge leo, baada ya kuridhishwa na kazi yake langoni.
Muwonge
amekuwa akiidakia Uganda tangu mwanzo wa mashindano haya, alipompokea kipa
namba moja, Abbel Dhaira ambaye aliumia kipindi cha kwanza kwenye mechi ya
kwanza kabisa ya Kundi A dhidi ya Kenya.
Na katika
mechi tano hadi jana alizodaka, kipa huyo hajaruhusu bao hata moja hadi
anaipeleka The Cranes fainali, jambo ambalo limewavutia Simba SC na sasa
wanaitaka saini yake.
Wakati huo
huo, Simba imekosa fursa ya kufanya mazungumzo na kocha wa Malawi, Kinnah Phiri
ambaye amerejea kwao na timu yake baada ya kutolewa katika Robo Fainali na
Kenya Jumanne.
Simba
inamtaka Kinnah baada ya kuona haiwezi kuendelea na kocha wake wa sasa, Mserbia
Profesa Milovan Cirkovick, ambaye kwa sasa yupo kwao Serbia, tangu kumalizika
kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara, mwezi uliopita.