Na Prince Akbar
SIMBA
imetwaa nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu
zenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya
kuitandika Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 3-0.
Hadi
mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 23 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam, Simba ilikuwa mbele kwa
bao 1-0.
Mabao yote
ya washindi katika mechi hiyo yalifungwa na Ramadhan Mkipalamoto. Mfungaji
alifunga bao la kwanza dakika ya 43 wakati mengine alipachika dakika za 57 na
70. Kwa kunyakua nafasi ya tatu, Simba imeondoka na kitita cha sh. 500,000.
Mechi ya
fainali ya michuano hiyo kati ya Azam ya Dar es Salaam na Coastal Union ya
Tanga itachezwa leo (Desemba 23 mwaka huu)
saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Mbali ya
kombe, bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa
kupitia maji Uhai atapata sh. milioni 1.5 wakati makamu bingwa atazawadiwa sh.
milioni 1.
Timu
iliyoonesha zaidi mchezo wa kiungwana (fair play) itapata sh. 400,000, mchezaji
bora wa mashindano sh. 350,000, mfungaji bora sh. 300,000 na kipa bora sh.
300,000. Naye kocha bora katika mashindano hayo atazawadiwa sh. 300,000 kama
itakavyokuwa kwa refa bora.