Kaburu kushoto wakati anamkabidhi jezi Ngassa baada ya kusaini kwa mkopo Simba |
Na Mahmoud Zubeiry
MAKAMU
Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema klabu yake haiku
tayari kufanya mazungumzo na Azam FC, kuhusu suala la kuuzwa kwa mchezaji Mrisho
Ngassa katika klabu ya El Merreikh ya Sudan, kwa sababu hawatendewi uungwana na
klabu hiyo.
Kaburu
ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, klabu yake iliingia mkataba na Azam FC
kwa kununua haki zote za huduma za Ngassa kwa mwaka mmoja, hadi Mei 21 mwakani,
ikilipa Sh. Milioni 25 kama ada ya kumtumia mchezaji huyo kwa mwaka mmoja pamoja
na kumlipa mchezaji haki zake zote stahiki za kimkataba ikiwemo mshahara wake.
Kaburu
amesema Azam bila ya kuzingatia mkataba iliousaini na Simba SC, na matakwa ya
FIFA yanayohusu mkopo, iliamua kutangaza kumuuza Ngassa bila ya kuihusisha Simba
wakati ikijua kuwa ilikuwa na Mkataba na Simba SC ambayo ameishaichezea katika
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara.
“Kitendo cha
Azam FC kuongea na Klabu ya El Merreikh FC na kuweka makubaliano ya mauzo ya
mchezaji na kumtangaza kuwa kimemuuza mchezaji Ngassa bila ya kuihusisha Simba
SC, na baadaye kuiandikia klabu ya Simba kuwa kimeamua kumrudisha mchezaji
Ngassa Azam, wakati ikijua kuwa ina mkataba na Simba SC ni uvunjifu mkubwa wa
taratibu na umeleta athari kubwa kwenye klabu yetu,”alisema Kaburu na kuongeza;
“Tayari
Simba SC ilikwishatuma malalamiko TFF na kupeleka pingamizi lake juu ya sulala
hili kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, ambapo imeamuliwa kuwa suala hili liende
kwenye Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezaji likapatiwe ufumbuzi,”alisema.
Amesema Simba
imekuwa ni klabu yenye kuangalia zaidi maslahi ya wachezaji na haina
kipingamizi kwa kuwaruhusu wachezaji wake kutoka pindi wanapopata timu nje ya
nchi kama utaratibu unafuatwa.
Kaburu
amesema Simba SC ilikuwa tayari kukaa mezani na Azam kwa mazungumzo, lakini kwa
kuwa Azam haipo tayari kutambua haki za Simba SC na imekuwa ikilitekeleza suala
hili kiholela, hivyo haioni sababu za kuzungumza na Azam FC na kuliacha suala
hili liende kwenye Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezaji kama TFF
ilivyoagiza.