Mussa Mudde |
Na Princess Asia
SIMBA SC
imesema kwamba Mussa Mudde ni miongoni mwa wachezaji wake wa kigeni wanne
ilionao kwa sasa na imeshangazwa sana na habari zilizoandikwa katika tovuti ya
supersport.com ya Afrika Kusini zikisema kwamba anarejea Sofapaka.
Akizungumza
kwa simu na BIN ZUBEIRY jana kutoka Uingereza, Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alisema kwamba Mudde ana mkataba wa
miaka miwili na Wekundu hao wa Msimbazi.
“Nashangaa
hizo habari wamezitoa wapi, huyu ni mchezaji wetu na mimi nilipoondoka Dar es
Salaam nilimuacha pale, ni vema wakati mwingine wakawa wanawasiliana na sisi
pia kutuuliza,”alisema Hans Poppe.
Wiki hii,
supersport.com imeandika kwamba Mudde anarejea Sofapaka baada ya kuona mambo
hayamuendei vizuri Simba SC.
Tovuti hiyo
ilimnukuu na rais wa Sofapaka, Elly Kalekwa ambaye alisema kwamba ameingia
mkataba wa miaka miwili na kiungo huyo mkabaji wa Mganda arejee Nairobi.
Mbali na
Mudde, wachezaji wengine wa kigeni ambao hadi sasa wana uhakika wa kuvaa jezi
za Simba SC ni kipa Abbel Dhaira, mshambuliaji Emmanuel Okwi wote kutoka Uganda
pia na beki Komalbil Keita kutoka Mali.
Kutoka
kikosi cha Simba kilichocheza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, wachezaji Felix
Sunzu kutoka Zambia, Daniel Akuffo kutoka Ghana na beki Paschal Ochieng kutoka
Kenya, wametupiwa virago.
Mudde
alisajiliwa tangu mwanzo wa msimu, lakini akaenguliwa kutokana na kuwa majeruhi
na hakucheza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, wakati Dhaira pia amesajiliwa wiki
iliyopita ili kuanza kazi Januari.