Owino |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya
Simba SC ya Dar es Salaam imesitisha mpango wa kumsajili beki wa kimataifa wa
Uganda, Joseph Owino kutoka Azam FC pia ya Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN
ZUBEIRY jana mjini Kampala, Uganda kwamba sababu za kuachana na beki
huyo na baada ya kufanyia tathmini kikosi chao na kuona hawahitaji beki, bali
wachezaji wa nafasi nyingine.
Simba SC
ilikwishafikia makubaliano na Azam FC kwa ajili ya kumsajili huyo, tena
wakibadilishana na kiungo Uhuru Suleiman na kuhusu dili hilo, Hans Poppe
alisema; “Wao sasa watatulipa tu ada ya uhamisho wa Uhuru, basi waka na Owino
wao,”alisema.
Tayari Uhuru
amekwishaanza kazi Azam FC na anafurahia maisha mapya katika klabu hiyo yenye
maskani yake maskani yake, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa sasa
Simba iko mbioni kusajili wachezaji wawili wa timu ya taifa ya Uganda, The
Cranes, kipa Hamza Muwonge na mshambuliaji Brian Umony, ingawa suala la kocha
wa Malawi, Kinnah Phiri halijakaa vizuri bado.
BIN ZUBEIRY juzi ilishuhudia mazungumzo kati ya
Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili
ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe na mshambuliaji huyo wa zamani wa SuperSport
United ya Afrika Kusini kwenye hoteli ya Sheraton mjini Kampala.
Muwonge
amekuwa akiidakia Uganda tangu mwanzo wa mashindano haya, alipompokea kipa
namba moja, Abbel Dhaira ambaye aliumia kipindi cha kwanza kwenye mechi ya
kwanza kabisa ya Kundi A dhidi ya Kenya.
Na katika
mechi tano hadi juzi alizodaka, kipa huyo hajaruhusu bao hata moja hadi
anaipeleka The Cranes fainali, jambo ambalo limewavutia Simba SC na sasa
wanaitaka saini yake.
Simba pia
imemtema mshambuliaji wake wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr.
kutokana na kuomba yeye mwenyewe na uongozi wa klabu hiyo kuridhia.
Sunzu
alisajiliwa Simba SC Julai 25 mwaka jana, akitokea El Hilal ya Sudan akisaini
mkataba wa miaka miwili kwa dola za Kimarekani 35,000 na mshahara wa dola
3,000.
Kutemwa kwa
Sunzu kunafanya idadi ya wachezaji wa kigeni waliotemwa Simba kufika watatu,
baada ya awali kutemwa beki Paschal Ochieng kutoka Kenya na mshambuliaji Daniel
Akuffo kutoka Ghana.
Simba
inamrejesha kikosini Mussa Mudde na kusaini Waganda wapya wawili, kipa Hamza
Muwonge na mshambuliaji Brian Umony, ambao wataungana na Mganda mwenzao kwenye
klabu hiyo, Emmanuel Okwi kufanya idadi ya wageni watano kwa mujibu wa kanuni
za Bara.