Baadhi ya wachezaji wa Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
KIKOSI cha Simba
SC kinaondoka kesho Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano ya
Kombe la Mapinduzi, michuano inyaonza Jumanne.
Makamu Mwenyekiti
wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba
timu hiyo itakuwa huko hadi baada ya mashindano, Januari 12 ndipo itaenda Oman
kwa ziara ya wiki mbili.
Simba SC
jana ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kufungwa mabao 3-0 na Tusker ya Kenya kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika
mchezo huo, uliochezeshwa vema na refa Hashim Abdallah, hadi mapumziko, tayari
Tusker walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Jesse Were dakika ya
37 na 45.
Mabao yote
yalitokana na udhaifu wa safu ya ulinzi ya Simba, ambayo hii leo iliongozwa na
beki kutoka Mali, Komabil Keita kiasi cha kufikia mfungaji anafunga akiwa
amebaki anatazamana na kipa.
Simba
ilikuwa ikishambulia kutokea pembeni, lakini mipira mingi mirefu iliyokuwa
inamiminwa langoni mwa Tusker ilikuwa inaokolewa na mabeki warefu wa klabu hiyo
bingwa ya Kenya, wakiongozwa na beki wa zamani wa Yanga, Joseph Shikokoti.
Kipindi cha
pili, Tusker walirudi kwa nguvu tena na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya
54, mfungaji Frederick Onyango.
Simba pamoja
na kufanya mabadiliko, ikiwatoa Haruna Shamte, Haruna Athumani, Paul Ngalema,
Mussa Mudde, Abdallah Seseme, Abdallah Juma, Ramadhani Chombo na Kiggi Makassy
na kuwaingiza Miraj Adam, Hassan Isihaka, Emily Ngeta, Jonas Mkude, Salim
Kinje, Haruna Moshi, Ramadhani Singano, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Edward
Christopher, haikuweza kupata hata bao la kufutia machozi.
Nassor
Masoud aliingia kuchukua nafasi ya Shamte, lakini naye akaumia na kutoka nafasi
yake ikichukuliwa na kinda wa Simba, B, Masele Kaheza.