Kikosi cha Simba kilichocheza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara |
Na Mahmoud Zubeiry
MABINGWA wa
Tanzania Bara, Simba SC wanatarajiwa kwenda Oman kuweka kambi ya kujiandaa na
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Habari kutoka
ndani ya Simba, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata, zimesema
kwamba Simba itakwenda nchini humo kwa mwaliko wa klabu kongwe ya huko, Fanja
FC.
Ikiwa huko,
Simba itacheza pia mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu tishio katika Ligi Kuu
ya Oman, wakiwemo wenyeji wao hao, Fanja FC.
Simba
inakuwa timu ya tatu ya Ligi Kuu kuwa katika mpango wa ziara ya nje ya nchi,
baada ya wapinzani wao katika mbio za ubingwa msimu huu, Yanga na Azam nao
kutangaza ziara zao.
Wakati Azam
watakwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndani ya siku mbili hizi,
Yanga watakwenda Uturuki mwishoni mwa mwezi huu.
Mbali na
Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa, mapema Januari Simba na Yanga zitacheza pia Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, michuano ambayo itafanyika
mjini Kigali, Rwanda.
Yanga watakwenda
kama mabingwa watetezi, baada ya kutwaa Kombe hilo Julai mwaka huu mjini Dar es
Salaam, wakati Simba watakwenda kwa tiketi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano
hiyo, wakiwa mabingwa wa Bara.
Kwa miaka
miwili mfululizo, timu za Bara zinaonekana kurejesha utawala wake kwenye
michuano hiyo, kutokana na fainali mbili mfululizo zilizopita kuzikutanisha
timu za Tanzania tupu.
Mwaka 2011,
Yanga iliifunga Simba SC 1-0, bao pekee la Mghana Kenneth Asamoah na kutwaa
taji la nne, wakati mwaka huu Watoto hao wa Jangwani, walikutana na Azam FC
katika mchezo wa Kombe uwanjani na kushinda 2-0, mabao ya Hamisi Kiiza na Said
Bahanuzi.
Azam, Simba
na Yanga kwa sasa ndio washindani wa taji la Ligi Kuu nchini, ambao wanaonekana
kutaka kujiimarisha vizuri kabla ya kuanza kwa hatua ya lala salama ya ligi
hiyo.