David Obua kushoto na BIN ZUBEIRY Lugogo, Kampala jana |
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
SIMBA SC,
Azam na Yanga, kama wana jeuri wailete hapa Kampala, Uganda kugombea saini ya
mchezaji aliyekuwa anakipiga Ulaya.
Huyo si mwingine
zaidi ya kiungo wa kimataifa wa Uganda, David Obua ambaye amemaliza mkataba
wake katika klabu ya Hearts ya Ligi Kuu ya Scotland na hataki kuongeza, ingawa
pia amekuwa mgumu kuelezea mikakati yake mipya.
Akizungumza na
BIN
ZUBEIRY mjini hapa, Obua alisema kwamba amemaliza mkataba wake Hearts
na kwa sasa yupo tu nyumbani Kampala. Alipoulizwa kuhusu mikakati yake mipya,
Obua alisema; “Sina cha kusema,”.
David amekuwa
akifuatilia mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Tusker Challenge mjini hapa tangu yameanza Novemba 24 na jana alikuwapo Uwanja
wa Lugogo kushuhudia Zanzibar na Bara zinazotengeneza Muungano wa Tanzania
zikitinga Nusu Fainali.
David ni mtoto
marehemu Denis Obua, ambaye aliichezea Uganda katika Fainali za Kombe la Mataifa
ya Afrika mwaka 1978 na ana mdogo wake, Eric Obua ambaye pia anachezea The Cranes.
Mjomba wake,
John Akii-Bua aliweka rekodi ya kuwa bingwa wa kwanza Mganda wa Olimpiki kwa
kushinda mita 400 huku akiweka rekodi ya dunia ya kutumia muda wa dakika 47 na
sekunde 82 mwaka 1972 mjini Munich, Ujerumani.
David Obua,
alizaliwa Aprili 10 mwaka 1984 mjini Kampala, Uganda na kisoka aliibukia katika
klabu ya Polisi mwaka 1999, kabla ya mwaka 2001 kusajiliwa Express ‘Red Eagles’
alikocheza hadi mwaka 2002
alipohamia AS Port-Louis ya Mauritius ambako alicheza msimu mmoja na kurejea
Express alikocheza hadi 2005 alipohamia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Lakini pia,
David wakati anasoma Marekani, alizichezea kwa muda klabu za Raleigh na
Wilmington Hammerheads za nchini humo.
Mwaka 2008,
David alitua Ulaya katika klabu ya Hearts ambako hadi anamaliza mkataba wake
amecheza jumla ya mechi 91 na kuifungia mabao sita.
Tangu mwaka 2003,
Obua amekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda na katika kipindi chote hicho, ameichezea Cranes mechi 27 na
kuifungia mabao 14.