Liewig |
Na Princess Asia
WAKATI kocha
mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kuwasili leo saa 7.25 mchana,
kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi kinatarajiwa kuondoka leo kwenda visiwani
Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi.
Makamu
Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba, Liewig
ambaye ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa,
ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, atakapofika atasaini
mkataba na kuanza kazi mara moja.
Kaburu alisema
kocha huyo mwenye Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa
soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller,
atakwenda na timu Zanzibar.
Liewig pia
amehudhuria kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo
Kikuu cha Dijon.
Kwa upande
wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha
Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za
timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha
kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia
mwaka 1989 hadi 1990: alikuwa Meneja
Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi
1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez,
1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa
Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia
alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa
ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari
mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za
U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia
mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa
mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super
Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya
makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa
Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba
mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia.