Hussein Twaha wa Serengeti, akiwatoka wachezaji wa Kongo Brazzaville katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam. Picha kutoka Maktaba ya BIN ZUBEIRY |
Na Prince Akbar
NDOTO za
Watanzania kuishuhudia timu yao ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17,
Serengeti Boys inacheza Fainali za Afrika mwakani nchini Morocco, leo zimeota
mbawa baada ya kufungwa mabao 2-0 na wenyeji Kongo Brazaville mjini Brazaville,
Kongo, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1.
Hata hivyo, katika
mchezo huo wenyeji waliwafanyia vurugu Watanzania tangu mwanzo wa mchezo ili
kuwavuruga kisaikolojia, ingawa hata hivyo vijana walipigana uwanjani na
wanastahili sifa.
Katika vurugu
hizo, Meneja wa Serengeti alipigwa na mashabiki kabla ya mchezo na hata wakati mchezo
ukiendelea Kocha Msaidizi wa Serengeti, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ naye alipigwa
na Polisi wa Kongo.
Kwa ujumla
mazingira hayakuwa mazuri uwanjani na kutolewa kwa Serengeti leo hakukuwa kwa
kimchezo, bali ubabe wa Wakongo, ambao katika mchezo wa kwanza walipokewa vizuri
na kufanyiwa ukarimu wa hali ya juu mjini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Katika mchezo
wa awali, Serengeti ilishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bao pekee
la beki Mudathir Yahya Abbas kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita
22 na mpira kabla ya kutinga nyavuni ulimbabatiza beki mmoja wa Kongo na
kumpoteza njia kipa Ombandza Mpea Joe na kujaa nyavuni.
Faulo hiyo
ilitokana na kiungo wa Serengeti, Hussein Twaha Ibrahim ‘Messi’kuangushwa na
beki Okombi Francis wakati akiwa analekea kwenye eneo la hatari la Wakongo.