Na Bin Zubeiry |
MWENYEKITI
wa Kamati ya Kusaidia timu za soka za vijana za taifa, Ridhiwani Kikwete, jana
aliuzungumzia mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam na kuweka
bayana ni mbovu.
Ridhi alisema
wazi, mfumo haufai kwa sababu unategemea fedha za kuendesha klabu kutoka kwenye
mfuko wa mtu mmoja.
Akizungumza
wakati anatoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) jana katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo
mkoani Pwani, Kikwete alisema kwamba Yanga inahitaji kubadilika kutoka mfumo
huo.
Kikwete
alisema ni afadhali mfumo wa uendeshwaji wa mahasimu wao wa jadi, Simba SC,
ambao desturi yao ni kuchangishana.
“Nilijaribu
kufanya uchunguzi wa mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga, nikashangazwa ni
mfumo mbaya, kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja, afadhali Simba wao huwa
wanachangishana,”alisema.
Alichokisema
Ridhiwani ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM, NEC akiiwakilisha Wilaya ya Bagamoyo ni kitu ambacho kipo
wazi, kwamba Yanga bado haina msingi imara.
Na vema hili
limezungumzwa na mtu mzito mapema, kabla ya uongozi mpya wa klabu hiyo chini ya
Mwenyekiti wake, Alhaj Yussuf Manji haujamaliza hata mwaka mmoja, ili kama
viongozi wao ni wasikivu, waitafutie misingi imara klabu.
Lazima ifike
wakati, Yanga iweze kujiendesha bila kutegemea mfuko wa mtu, na hapo ndipo
itasaidia hata kuondoa ‘Miungu watu’ ndani ya klabu. Ndiyo, ndani ya Yanga kuna
watu wanataka kuabudiwa kila siku, wakijua wao ndiyo wenye uwezo wa kuifanya
timu isimame.
Hili haliko
sawa na kama alivyosema Ridhiwani, viongozi wapya wa Yanga wanatakiwa kuleta
mapinduzi katika klabu.
Yanga ni
klabu ambayo inaweza kujiendesha kutokana na ukweli kwamba ni taasisi kubwa,
ina rasilimali kuanzia ya watu na mali zisizohamishika.
Jengo la Mafia,
jengo la makao makuu ya klabu pale Jangwani pamoja na Uwanja wa Kaunda, vyote ni
vitegauchumi vikubwa sana vinavyoweza kuifanya Yanga ijiendeshe.
Ndiyo,
Mwenyekiti wa Yanga, Manji alimtambulisha mkandarasi wa kujenga upya Uwanja wa
Kaunda, lakini bado tunasubiri utekelezaji wake. Lakini pia, lazima iwekwe
bayana, mkandarasi huyo anajenga Uwanja huo kwa makubaliano yapi na ni nani
atakayegharamia fedha za ujenzi huo.
Na je, anajitolea
au anaikopesha klabu. Ndiyo, maana wana Yanga wasifurahie tu ahadi ya ujenzi wa
Uwanja bila kujua kesho nini kitafuata. Wakati, fulani mwanachama mmoja wa
Yanga, Abeid Falcons alitaka kuukarabati Uwanja wa Kaunda, lakini akazuiwa na
uongozi chini ya Mwenyekiti wa wakati huo, Wakili Imani Madega, kwa sababu
ilikuwa ni hatari kwa klabu.
Kila siku
nasema, Yanga si mali ya mtu. Ni mali ya watu, hivyo isitokee watu kwa sababu
tu wamepewa dhamana ya kuongoza wakajisahau na kuichukulia kama ile ni mali
yao. Hapana.
Leo mambo
bado yanakwenda holela tu Yanga na huwezi kuona dalili za mabadiliko kutokana
na uongozi mpya. Wana Yanga bado wananunua jezi, kalenda na bidhaa nyingine kibao
zenye nembo ya klabu, lakini haijulikani klabu inanufaika vipi.
Iko wapi
mikataba ya tenda hizi- zilitangazwa lini? Tuachane na hayo, Yanga inapata nini
kutokana na mauzo ya bidhaa hizo?
Miezi miwili
iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alitoa taarifa ya mapato
na matumuzi ya kipindi cha miezi mitatu cha kuwapo kwao madarakani, ikaonyesha
Yanga inajiendesha kwa hasara- maana yake inategemea mfuko wa mtu.
Lakini kwa
nini klabu kubwa kama hiyo ijiendeshe kwa hasara? Bado siku chache baadaye,
anaitisha Mkutano kutangaza kuingia mkataba na kampuni ya Prime Time Promotions
isimamie mkutano Mkuu na kuiandalia klabu mechi za kirafiki za kimataifa kwa
mkataba wa Sh Milioni 105.
Huu ni
mzaha, Yanga ina uwezo kuingiza Sh. Milioni 300 au zaidi katika mechi moja tu
ya maana ya kirafiki itakayocheza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, iweje leo
Prime Time ipewe tenda ya kuandaa mechi ambazo idadi yake haijulikani kwa
Milioni 105 tu?
Hizi ni
dalili tosha za wanachama wa Yanga kuanza kupata shaka juu ya uongozi wao mpya,
kama kweli utaweza kuivusha klabu katika hatua nyingine.
Kama unashindwa
kuongoza Yanga, yenye rasimimali kibao, kweli utaweza kuongoza timu kama Toto
Africans?
Yuko mtu
anaitwa Rahim Kangezi ‘Zamunda’, huyu jamaa anavyoteseka na African Lyon unaona
kabisa akiipata timu kama Yanga, ataifikisha mbali sana.
Zamunda ana
mipango na ni mtendaji, kitu ambacho viongozi wa Yanga wa sasa kama wanakosa
hivi. Lakini bado viongozi wa Yanga
wanaweza kuwa karibu na Zamunda ili kujifunza kwa manufaa ya Yanga.
Ukienda kwenye
masuala mengine ya kiutendaji Yanga, bado ni vurugu tupu. Makomandoo bado
wanakumbatiwa, usajili mwingine unafanyika usio na tija kwa klabu, ili mradi tu
kuna watu wamepewa dhamana, wao ndio wenye mamlaka na hakuna wa kuwaambia kitu.
Ama kwa
hakika Ridhiwani ameona mbali sana, mfumo wa uendeshaji Yanga ni mbovu. Tena
kupita maelezo.