Mwenyekiti aliyemaliza muda wake TAREFA, Alhaj Ismail Aden rage |
Na Prince Akbar
SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF) limeupongeza uongozi mpya wa Chama cha Soka Tabora
(TAREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Desemba 22 mwaka huu).
Ofisa Habari
wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba, ushindi
waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa TAREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo
huo mkoani Tabora.
Amesema TFF
inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAREFA chini ya
uenyekiti wa Yusuf Kitumbo aliyeshinda kwa kura 16 dhidi ya nane za Musa
Ntimizi, na Paul Werema ambaye hakupata kura.
“Uongozi huo
mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za
mpira wa miguu mkoani Tabora kwa kuzingatia katiba ya TAREFA pamoja na vyombo
vya mpira wa miguu vilivyo juu yake,”.
“Pia tunatoa
pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa
kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF,”alisema Wambura.
Viongozi
waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Yusuf Kitumbo (Mwenyekiti), Fate Remtulla
(Katibu), Dick Mlimuka (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Razak Irumba (Mwakilishi
wa Klabu TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Eric Kabepele na
Mwalimu Sizya.
Wakati huo
huo: Chama cha Soka ya Wanawake Tanzania (TWFA) kimetoa tuzo kwa Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na Meneja wa timu
ya Taifa (Twiga Stars), Furaha Francis kutokana na mchango wao katika
kuendeleza mchezo huo.
Tuzo hizo
zilitolewa katika Mkutano wa Uchaguzi wa TWFA uliofanyika Desemba 19 mwaka huu
mjini Morogoro kutokana na mchango wao katika kuendeleza mpira wa miguu kwa
wanawake nchini.
“Ni dhahiri
kazi ya kuendeleza soka ya wanawake ni wajibu wa Shirikisho (TFF), lakini Rais
wa TFF alitoa kipaumbele zaidi na alijitoa kuhakikisha misingi imara ya
kuendeleza soka ya wanawake inawekwa,” alisema Mwenyekiti wa TWFA, Lina Kessy.
Pia Mkutano
huo ulitambua na kumpa tuzo Furaha Francis ambaye amekuwa Meneja wa Twiga Stars
kwa miaka minane mfululizo. Licha ya kuwa Meneja wa Twiga Stars, ametumia muda
wake na kujitoa katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake.
TWFA
itaendelea kutumia michango yao katika mpira wa miguu kwa wanawake nchini.