Kim Poulsen kulia na Msaidizi wake Marsh kushoto |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KOCHA wa
Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amesema kwamba anamuweka benchi
kwa sasa kiungo mshambuliaji Simon Msuva, katika Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati, kwa sababu Amri Kiemba anafanya kazi nzuri katika kikosi cha
kwanza.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY katika mahojiano maalum jana, Uwanja wa Mandela, Namboole,
alisema kwamba alipompa nafasi ya Kiemba amefanya kazi nzuri ambayo imemvutia
na kuamua kuendelea kumtumia kwenye kikosi cha kwanza.
“Najua Msuva
ni winga mzuri, ana kasi na anashambulia sana, lakini hata Kiemba anafanya kazi
nzuri, tena kama jana (juzi) amefunga hadi bao, kwa kweli ananivutia na
anafanya kazi yake vizuri,”alisema.
Msuva
alianza katika mechi mbili za mwanzoni za Kundi B kwenye michuano hii, dhidi ya
Sudan na Burundi, lakini baada ya hapo amemalizia benchi dakika zote 180 katika
mechi kwenye mechi mbili zilizofuata dhidi ya Somalia na Rwanda.
Hata hivyo,
Kim alisema bado Msuva anaweza akatokea benchi wakati wowote na kwenda kuongeza
nguvu katika kikosi cha Kilimanjaro Stars hasa katika hatua ngumu ambayo
michuano hii imefikia.
Stars
imefika Nusu Fainali na kesho itamenyana na wenyeji Uganda, Uwanja wa Mandela,
Namboole, kuanzia saa 12: jioni, mchezo ambao utatanguliwa na Nusu Fainali
nyingine kati ya Kenya na Zanzibar, itakayoanza saa 10:00 jioni.
Stars
ilitinga Nusu Fainali, baada ya kuifunga Rwanda mabao 2-0 juzi kwenye Uwanja wa
Lugogo mjini hapa, ambayo yalitiwa kimiani na Amri Kiemba na John Bocco.
Awali ya
hapo, Stars ilifuzu Robo Fainali kama mshindi wa pili kwenye kundi lake, nyuma
ya Burundi baada ya kujikusanyia pointi sita, yaani ikishinda mechi mbili 2-0
na Sudan na 7-0 na Somalia, wakati yenyewe ilifungwa 1-0 Mbayuwayu wa Bujumbura.