Ssentongo aliyepiga mawili leo |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
NDOTO za
Tanzania Bara kurejea nyumbani na Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati,
CECAFA Tusker Challenge zimeyeyuka baada ya usiku huu kufungwa na wenyeji
Uganda mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
Kwa matokeo
hayo, Uganda itamenyana na majirani zao na wapinzani wao wakubwa, Kenya katika
fainali Jumamosi, ambao katika mchezo wa kwanza waliitoa kwa mikwaju ya penalti
4-2 Zanzibar, kufuatia sare ya jumla ya 2-2 ndani ya dakika 120.
Zanzibar na
Bara zitamenyana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu siku hiyo hiyo ya
Jumamosi kwenye Uwanja wa Namboole.
Hadi
mapumziko, Uganda walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Emmanuel
Okwi dakika ya 11, baada ta kuuwahi mpira mrefu uliopigwa na kipa wake, Hamza
Muwonge na kufumua shuti kali la umbali wa mita 19, ambalo lilimshinda kipa
Juma Kaseja.
Baada ya bao
hilo, Okwi aliumia na kutoka nje dakika ya 36 nafasi yake ikichukuliwa na
Hamisi Kiiza.
Uganda ndio
waliouanza mchezo huo kwa kasi na kulitia misukosuko lango la Stars kwa
takriban dakika 10 mfululizo, lakini baada ya hapo timu hizo zikaanza
kushambuliana kwa zamu.
Timu zote
zilikuwa zikishambulia kutokea pembeni, lakini Uganda ndio walioonekana kuzalisha
mashambulizi ya hatari zaidi.
Kipa na
Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alitoka uwanjani baada ya dakika 45 za kipindi
cha kwanza akilaumiana na mabeki wake kwa kufungwa bao la kutanguliwa.
Kipindi cha
pili, Waganda walirudi na moto wao tena na kufanikiwa na kupata bao la pili
dakika ya 51, safari hii Robert Ssentongo akimtungua Kaseja, baada ya mabeki wa
Stars kudhani ameotea.
Pamoja na
kufungwa bao la pili, Stars waliendelea kucheza kwa juhudi, ingawa Waganda
waliendelea kutawala mchezo.
Mpira
uliotemwa na Juma Kaseja kufuatia shuti la Moses Oloya, ulimkuta Ssentongo dakika
ya 71 akaukwamisha nyavuni na kuipatia The Cranes bao la tatu. Kutoka hapo,
hali ilikuwa mbaya kwa Stars.
Zikiwa zimesalia
dakika tano mchezo kumalizika, taa za Uwanja wa Mandela zilizimika, lakini
baada ya jitihada za pamoja za FUFA, CECAFA na uongozi wa Uwanja, ziliwaka
baada ya dakika saba na mchezo kuendelea hadi filimbi ya mwisho.
Katika mchezo
huo, kikosi cha Uganda kilikuwa;
Hamza Muwonge, Iguma Dennis, Godfrey Walusimbi, Henry Kalungi, Isaac Isinde,
Hassan Wasswa, Geoffrey Kizito, Moses Oloya, Robert Ssentongo, Emanuel
Okwi/Hamisi Kiiza dk36 na Joseph Ochoya/Brian Majwega dk79.
Tanzania; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir
Maftah, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Franko Domayo, Amri Kiemba, Salum
Abubakar/Athumani Iddi dk63, Mwinyi Kazimoto, John Bocco na Mrisho Ngassa.