Na Princess Asia
MECHI za Nusu
fainali ya michuano ya Kombe la Uhai 2012 inayoshirikisha timu za vijana wenye
umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom zitachezwa kesho
(Desemba 21 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Nusu fainali
ya kwanza ya michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa
kupitia maji Uhai itazikutanisha timu za Mtibwa Sugar ya Morogoro na Azam na
itafanyika kuanzia saa 2 kamili asubuhi.
Simba na
Coastal Union zitacheza nusu fainali ya pili kuanzia saa 10 kamili jioni kwenye
uwanja huo huo. Mtibwa Sugar imepata tiketi ya nusu fainali baada ya kuichapa
African Lyon mabao 3-1 wakati Simba iliilaza Oljoro JKT mabao 2-0.
Nayo Azam
iliindoa JKT Ruvu kwenye robo fainali kwa bao 1-0 huku Coastal Union ikipata
ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mechi ya mwisho ya robo
fainali.
Mechi ya
fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili (Desemba 23
mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Mechi ya
mshindi wa tatu itaanza saa 2 kamili asubuhi wakati ya fainali itakuwa saa 10
kamili jioni.