Niyonzima kushoto akibadilishana bendera na nahodha wa Bara, Juma Kaseja Lugogo jana |
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
NAHODHA wa
Rwanda, Haruna Niyonzima amewatabiria Tanzania Bara kutwaa ubingwa wa Kombe la
Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwaka huu.
Kiungo huyo
wa Yanga SC ya Dar es Salaam aliyasema hayo baada ya mechi ya Robo Fainali jana
Uwanja wa Lugogo baina ya nchi hizo mbili, ambayo Bara walishinda mabao 2-0.
“Tumekubaliana
na matokeo, sisi tulishindwa kutumia nafasi, wenzetu walicheza vizuri na
walitumia nafasi, tunakubali huo ndio mpira sisi tumetolewa,”alisema.
Niyonzima aliisifu
Bara kucheza vizuri na kwa nidhamu ya hali ya juu na akasema kama wataendelea
hivyo, basi watarejea na Kombe Dar es Salaam. “Kila mtu alikuwa anatekeleza
majukumu yake vizuri uwanjani na kwa kweli mimi nawapongeza,”alisema.
Bara ilifanikiwa
kuingia Nusu baada ya kuilaza Rwanda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Lugogo mjini
hapa.
Hadi
mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri
Kiemba, dakika mya 33 akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza
wachezaji wawili wa Rwanda kabla ya kutoa pasi maridadi.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John
Raphael Bocco ‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na
aliwafanya waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.
Katika hicho
kipindi cha kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya
Jean Claude Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19
Jean Baptiste Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.
Stars pamoja
na kufunga bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri
ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha
na ikawapita wote.
Ngassa tena,
katika dakika ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda
nje sentimita chache.
Kipindi cha
pili Stars walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na
Rwanda nao waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.
Hata hivyo,
walikuwa ni Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili dakika ya 53 baada ya
John Bocco kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti
kali la Mwinyi Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.