Na Princess Asia
TIMU za Azam
ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga ndizo zitakazoumana kwenye fainali
ya michuano ya Kombe la Uhai 2012 itakayochezwa kesho jioni kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Timu hizo
zimepata fursa hiyo baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali ya michuano
hiyo inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za
Ligi Kuu ya Vodacom jana. Michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim
Bakhresa kupitia maji Uhai.
Azam ndiyo
iliyokuwa ya kwanza kupata tiketi ya fainali baada ya kuitoa Mtibwa Sugar ya
Morogoro kwa mikwaju ya penalti 3-2. Matokeo ya dakika 90 yalikuwa bao 1-1.
Nayo Coastal Union iliivua ubingwa Simba kwa kuifunga mabao 2-1.
Mechi ya
fainali itaanza saa 10 kamili jioni, na itatanguliwa na ile ya kutafuta mshindi
wa tatu kati ya Mtibwa Sugar na Simba ambayo itachezwa saa 2 kamili asubuhi
kwenye uwanja huo huo.
Mbali ya
kombe, bingwa wa michuano hiyo atapata sh. milioni 1.5, makamu bingwa sh.
milioni 1 wakati mshindi wa tatu atajinyakulia sh. 500,000. Timu iliyoonesha
zaidi mchezo wa kiungwana (fair play) itapata sh. 400,000, mchezaji bora wa
mashindano sh. 350,000, mfungaji bora sh. 300,000 na kipa bora sh. 300,000.
Naye kocha
bora katika mashindano hayo atazawadiwa sh. 300,000 kama itakavyokuwa kwa refa
bora.