Umony |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
MSHAMBULIAJI
wa Uganda, Brian Umony amesema kwamba katika mechi mbili zilizobaki za Kombe la
Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge atajitahidi awapiku
wachezaji wa Tanzania, John Bocco na Mrisho Ngassa katika ufungaji wa mabao
kwenye michuano hiyo.
“Mimi nina
mabao matatu, wao kila mmoja ana mabao matano, sijakata tamaa, nitajitahidi
niwapiku, najua ni kazi ngumu, lakini nitajitahidi sana,”alisema mchezaji huyo
ambaye ameonyesha nia ya kujiunga na Simba SC ya Dar es Salaam.
Akiizungumzia
mechi ya Nusu Fainali dhidi yao na Tanzania Bara kesho, Umony alisema anaamini
itakuwa ngumu sana, lakini watapambana kushinda.
“Tanzania
wana timu nzuri sana, ina wazoefu ambao mimi nawajua kama Mrisho Ngassa na Juma
Kaseja, kwa kweli mchezo utakuwa mgumu, itakuwa mechi nzuri sana yenye hadhi ya
fainali,”alisema Umony.
Brian
amerejea nyumbani Uganda na kujiunga na Express baada ya kumaliza mkataba wake,
Becamex Binh Duong F.C. ya Vietnam.
Mwaka 2009,
baada ya Simba kuzidiwa kete na SuperSport United ya Afrika Kusini kwa Umony,
ikamsajili Emmanuel Okwi aliyekuwa SC Villa wakati huo.
Umony
aliichezea Supersport United hadi 2010 alipohamia University of Pretoria ya
Afrika Kusini pia hadi mwaka 2011 alipohamia Portland Timbers ya Marekani kwa
mkopo na mwaka huu akatua Becamex Binh Duong F.C.
Tayari Umony
amesema anaweza kujiunga na Simba wakiafikiana naye dau.
WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE
2012
John Bocco Tanzania 5
Mrisho
Ngassa Tanzania 5
Brian Umony Uganda 3
Suleiman
Ndikumana Burundi 3 (1 penalti)
Chris
Nduwarugira Burundi 3
Geoffrey
Kizito Uganda 2
Robert
Ssentongo Uganda 2
Khamis Mcha Zanzibar 2
David
Ochieng Kenya 2
Clifton
Miheso Kenya 2
Dadi Birori Rwanda 2