Mhando, katibu wa TASWA |
Na Prince Akbar
KAMPUNI ya
Msama Promotions inayoandaa Tamasha la Pasaka imeahidi kutoa Sh. Milioni 1.5
kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA) utakaofanyika Bagamoyo mkoani Pwani wiki ijayo.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ambaye ndiye Mkurugenzi wa
kampuni hiyo amesema ushirikiano wake na
wanahabari umemsukuma kusaidia kiasi hicho cha fedha.
Msama
ameahidi kuendelea kushirikiana na TASWA kadri awezavyo na kwamba mafanikio ya
Tamasha la Pasaka yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na wanahabari.
“Kampuni
yangu ya Msama Promotions kupitia Tamasha la Pasaka tumeamua kuungana na
wanahabari katika kufanikisha mkutano wenu, tunaamini uhusiano wetu utaendelea
kuwa wa kupigiwa mfano,” ilisema sehemu ya taarifa ya TASWA jana ikimkariri
Msama.
Kwa upande
wake Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alishukuru kwa udhamini huo na kuomba
wengine wenye moyo wajitokeze kuwasaidia kwani bajeti yao ni Sh. Milioni 20.
Tayari kampuni ya simu za mkononi ya Zantel imeshatangaza udhamini wa Sh.
Milioni sita.
Mhando
alisema maandalizi ya Mkutano Mkuu wa TASWA utakaofanyika wiki ijayo Bagamoyo
mkoani Pwani yanaendelea vizuri na kwamba zaidi ya wanachama 100 wa TASWA na
wadau wengine wa TASWA wamethibitisha kushiriki.
Wakati huo
huo: TASWA imewapongeza wanachama wake Benny Kisaka na Zena Chande kwa
kufanikiwa kuwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kisaka
alishinda wadhida huo wiki iliyopita kupitia uchaguzi wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), wakati Chande alishika Jumatano katika
uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania (TWFA).
“Tunaamini
wajumbe wa Mkutano Mkuu DRFA na wale wa TWFA hawakufanya makosa, wamefanya
uamuzi sahihi na wamepata watu sahihi na makini na michango yao itakuwa yenye
tija kubwa kwa maendeleo la mpira wa miguu hapa nchini. Tunawatakia kila la
heri wanachama wetu hao katika changamoto mbalimbali watakazokutana nazo kwenye
nafasi zao hizo walizopata,”amesema Amir Mhando, Katibu Mkuu TASWA.