Mwaikimba DRC |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
MSHAMBULIAJI
mrefu, Gaudence Exavery Mwaikimba anayeng’ara kwenye michuano ya Kombe la Hisani
hapa DRC, amesema kwamba bado ana uwezo mkubwa wa kuisaidia timu yake ya taifa
ya Tanzania, Taifa Stars, lakini hawezi kuingilia maamuzi ya kocha Kim Poulsen.
Akizungumza na
BIN
ZUBEIRY mjini hapa jana, Mwaikimba alisema kwamba uwezo wake siku zote
upo juu kwa sababu ana kipaji na anajituma mazoezini, lakini hajui Kim
anamfikiria vipi.
“Tangu mimi
nimeibuka katika soka ya nchi hii, hakuna kocha ambaye alikuja kufundisha timu
ya taifa akaacha kuniita kwenye kikosi, nadhani hata huyu Kim bado hajaniona
tu, lakini mwenzake Jan Borge Poulsen aliniita,”alisema.
Mwaikimba alisema
hawezi kulazimishwa kuitwa timu ya taifa kwa sababu ile ni timu ya Watanzania
wote na Tanzania ina wachezaji wengi, ila roho itaendelea kumuuma kila timu
itakapokuwa ikifanya vibaya wakati yeye ana uwezo wa kuisaidia.
“Ni kweli
Tanzania ina washambuliaji wengi, lakini mimi ni wa kipekee, kama ninakuwa
kwenye timu na kocha akanitumia vizuri, lazima nitakuwa tishio. Sema tu tatizo
makocha wengi wa hapa hawajiamini na wanashindwa kufanya kazi zao vizuri,”alisema.
“Angalia
Stewart (Hall, kocha wa Azam) huyu hapa, ndiye kanisajili hapa Azam na hadi
kesho ananitumia na ananielekeza vizuri. Yaani mimi nauona umuhimu wangu kwake,
inakuwa rahisi mtu kufanya kazi,”alisema.
Katika mechi
tatu za mashindano ya Kombe la Hisani, Mwaikimba amefunga mabao mawili hadi sasa.
Mwaikimba alikuwa
mchezaji wa timu ya taifa kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, ingawa wakati fulani mwaka
2009 aliwahi kutemwa na kocha Mbrazil, Marcio Maximo baada ya kiwango chake
kushuka.
Na kushuka
kwa kiwango chake kulichangiwa na migogoro na kocha wa klabu yake ya zamani,
Profesa Dusan Savo Kondic raia wa Serbia, kiasi cha kufikia kuhama timu.