Gaudence Mwaikimba; Mfungaji bora Kombe la Hisani DRC |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
MSHAMBULIAJI
Gaudence Mwaikimba wa Azam amekuwa mfungaji wa mashindano ya Kombe la Hisani yaliyoandaliwa
na FECOFA, Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada
ya kumaliza na mabao matatu, akifuatiwa na Kipre Herman Tchetche na Ngulubi Kilua
wa Shark FC waliofunga mawili kila mmoja.
Jumla pamoja
na penalti za baada ya dakika 90 za mechi, Mwaikimba amefunga mabao matano, Kilua
matatu na Kipre matatu.
Hata hivyo,
kwa kuwa mashindano haya ni ya hisani, hakutakuwa na zawadi mwa bingwa wala
wachezaji bora, hivyo Mwaikimba anaondoka DRC na hadhi tu ya ufungaji bora.
Azam jana
iliwafunga wenyeji Dragons FC kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya
dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs mjini hapa na kutwaa Kombe. Azam walikuwa wa
kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kabla ya Dragons kusawazisha dakika ya
75.
Katika mikwaju
ya penalti, kipa Mwadini Ally alicheza mikwaju miwili ya Dragons, wakati Gaudence
Mwaikimba, Himid Mao, Joackins Atudo na Samih Hajji Nuhu walifunga penalti za Azam.
Hata hivyo,
Azam jana hawakukabidhiwa Kombe uwanjani hapo baada ya waandaji kusema wanakwenda
kulipamba kwanza, hivyo sherehe za makabidhiano ya Kombe zinaweza kufanyika leo.
Azam iliingia
fainali, baada ya juzi kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya
hapa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs. Azam inatarajiwa
kuondoka hapa kesho mchana kurejea Dar es Salaam.